Michezo

Mashabiki wafurahia mechi za Super 8 Nairobi

April 23rd, 2019 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

MASHABIKI walipata burudani ya kutosha msimu wa Pasaka kutokana na mechi mbali mbali za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Super 8.

Kwenye mechi hizo zilizochezewa katika viwanja tofauti vya Kaunti ya Nairobi na viungani, timu za MASA, Githurai All-Stars na Makadara Junior League SA, ziliandikisha ushindi dhidi ya wapinzani wao.

MASA waliichapa Rongai All-Stars 3-1, Jumamosi katika mechi iliyochezewa uwanja wa Makongeni.

Mchezaji Gilbert Mogaka (kulia) wa MASA na Glen Nelson (kushoto) wa Rongai All Stars wakiwania mpira wakati wa mechi yao ya kuwania ubingwa wa Super 8 Jumamosi uwanjani Makongeni. MASA ilishinda kwa 3-1. Picha/ John Ashihundu

Githurai All-Stars waliandikisha ushindi mkubwa wa 5-0 dhidi ya Huruma Kona katika mechi iliyochezewa Stima Club, ushindi ambao umewapandisha hadi nafasi ya pili jedwalini kutokana na pointi 13.

Ugani Drive Inn, bao la Erick Kariuki alilofunga dakika ya 46 liliiwezesha Makadara Junior League SA kuibwaga Metro Sports, ambao sasa wameshuka hadi nafasi ya 12 baada ya kujikusanyia pointi nane.

Kuambulia patupu mechi tatu

MASA walipata ushindi wa juzi baada ya awali kwenda mechi tatu bila kushinda.

Vijana hao wa kocha Hosea Akala walijipatia bao la kwanza kupitia kwa kiungo Gona Abdalla, kabla ya Rongai kusawazisha dakika ya 38 kupitia kwa Samuel Kapen.

Kipa Halkano Guyo wa Rongai alisababisha penalti baada ya kucheza rafu. Chris Oduor alifunga penalti hiyo na kufanya timu yake kuwa kifua mbele kwa 2-1 kufikia wakati wa mapumziko.

Abdalla aliongeza bao la tatu dakika ya 66 baada ya kuonana vyema na Oduor.

MASA wanakamata nafasi ya tisa, sawa na Rongai lakini MASA wako mbele kutokana na wingi wa mabao, huku kila moja ikiwa imecheza mechi saba.

“Nimefurahia matokeo yetu mazuri ambayo yamechangiwa na maandalizi mema,” alisema kocha Akala.