Mashabiki wamtaka Rachier ajiuzulu kwa kukiri ni Freemason

Mashabiki wamtaka Rachier ajiuzulu kwa kukiri ni Freemason

NA CECIL ODONGO

MWENYEKITI wa Gor Mahia Ambrose Dickens Otieno Amollo Rachier ameanza kuandamwa na shinikizo zinazomtaka ajiuzulu baada ya kikiri hadharani kuwa anajihusisha na imani isiyoeleweka almaarufu Freemasonry.

Kupitia mahojiano yaliyopeperushwa katika runinga ya NTV mnamo Jumapili, Rachier alikiri hadharani kuwa yupo kwenye kundi la watu wenye imani hiyo ambayo wengi wamekuwa wakiihusisha na uabudu wa shetani.

Rachier alifichua kuwa alikumbatia dini hiyo mnamo 1994 baada ya kuingizwa na rafiki yake na dhana kuwa ni uabuni wa shetani ni potovu.

Alifafanua kuwa hawashiriki au kutoa kafara za binadamu huku akifichua wao hujikita sana katika utoaji wa misaada kwa wasiojiweza.

Kukiri kwa Rachier kuwa anajihusisha imani hiyo kuliwashangaza wengi huku baadhi ya mashabiki wa Gor sasa wakimtaka aondoke na asijihusishe na timu yao.

Hapo jana Jumatatu, Katibu wa Gor Sam Ochola alisema kuwa umma wote wa Gor haufai kuhusishwa na imani hiyo isiyoeleweka akisema hayo ni maisha ya Rachier kama mtu binafsi.

“Kama kamati kuu ya Gor, tulifuatilia simulizi ya mwenyekiti wetu katika runinga kama Wakenya wengine. Hata hivyo, wachezaji, waajiriwa na wote wanaoifanyia Gor kazi hawapo kwenye imani hiyo. Tunawaomba mashabiki wetu wasalie watulivu wakisubiri uamuzi ambao tutauchukua kuhusu suala hili,” akasema Ochola kupitia taarifa.

Kando na Ochola na Rachier, maafisa wengine wa ngazi ya juu kambini mwa Gor Mahia ni Francis Wasuna ambaye ni Naibu Mwenyekiti na mwekahazina Dolphina Odhiambo.

Mitandaoni baadhi ya mashabiki walimtaka Rachier ajiuzulu kwa kuwa imani yake inatoa taswira kuwa Gor pia imekumbatia imani hiyo ilhali si kweli.

Shabiki nambari moja wa Gor Mahia Jared Otieno maarufu kama Jaro Soja pia aliunga kauli ya Ochola akisema kuwa wanaohusisha Gor Mahia na imani ya Rachier wanakosea.

Rachier, wakili maarufu Nairobi alichukua usukani mnamo 2009 kutoka kwa aliyekuwa Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Nchini Erasrus Okul.

Akiwa usukani, Rachier ameongoza Gor kutwaa mataji saba ya Ligi Kuu ( KPL), kufika katika hatua ya robot fainali ya Kombe la Mashirikisho Afrika na pia kushiriki mechi za Klabu Bingwa Afrika pamoja na kushinda mataji mengine kwenye mashindano mbalimbali.

Rachier alitetea wadhifa wake bila kupingwa kwenye uchaguzi ulioandaliwa mnamo 2020 na anatarajiwa kuondoka mamlakani mnamo 2024.

Baada ya kuchaguliwa, aliahidi kuwa hatatetea wadhifa wake mnamo 2024.

  • Tags

You can share this post!

Mbona mwasho mkali kwenye chuchu zangu?

Liverpool na Spurs kujinyanyua UEFA

T L