Mashabiki wapokea kikosi cha Italia kwa shangwe na mbwembwe za kila aina baada ya kushinda taji la Euro

Mashabiki wapokea kikosi cha Italia kwa shangwe na mbwembwe za kila aina baada ya kushinda taji la Euro

Na MASHIRIKA

ILIKUWA mbwembwe na vifijo vya kila sampuli miongoni mwa mashabiki waliojitokeza kwenye barabara na vichochoro vya miji mbalimbali ya Italia kusherehekea ushindi wa kikosi chao kilichokung’uta Uingereza 3-2 kwenye penalti na kutwaa taji la Euro mnamo Julai 11, 2021.

Kikosi cha Italia kiliwasili nchini mwao alfajiri ya Julai 12, 2021 na kupokelewa na umati mkubwa wa mashabiki waliokongamana katika uwanja wa ndege wa Fiumicino.

Taji hilo lilikuwa la kwanza kwa Italia kutia kapuni tangu watawazwe wafalme wa Euro mnamo 1968 baada ya kucharaza Yugoslavia 2-0 jijini Roma.

Mshindi wa gozi kati ya Italia na Uingereza mnamo Jumapili usiku uwanjani Wembley aliamuliwa kupitia penalti baada ya pande zote mbili kuambulia sare ya 1-1 kufikia mwisho wa muda wa ziada.

Beki Luke Shaw wa Manchester United aliwaweka Uingereza kifua mbele mwanzoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya Leonardo Bonucci kusawazishia Italia waliojikuta nyuma kwa mara ya kwanza kwenye kampeni za Euro mwaka huu. Bao hilo la Shaw lilikuwa lake la kwanza ndani ya jezi ya Uingereza na ndilo la haraka zaidi kuwahi kufumwa wavuni katika fainali ya Euro.

Akiwa na umri wa miaka 34 na siku 71, Bonucci sasa ndiye sogora mkongwe zaidi kuwahi kufunga bao katika fainali ya Euro. Nahodha huyo msaidizi wa Juventus ndiye mchezaji wa pili mwenye umri mkubwa mno kuwahi kutikisa nyavu za wapinzani kwenye fainali ya soka ya haiba tangu Nils Liedholm afungie Uswidi dhidi ya Brazil kwenye Kombe la Dunia mnamo 1958 akiwa na miaka 35 na siku 264.

Chini ya kocha Roberto Mancini, Italia waliendeleza rekodi ya kutoshindwa katika mechi 34 mfululizo tangu wapigwe 1-0 na Ureno kwenye gozi la Uefa Nations League mnamo Septemba 2018.

Aidha, kikosi hicho ndicho cha kwanza kuwahi kushinda taji la Euro baada ya kutawala michuano miwili kupitia penalti. Kabla ya kushuka dimbani kumenyana na Uingereza, miamba hao walikuwa wamedengua Uhispania kwa penalti 4-2 baada ya kuambulia sare ya 1-1 kwenye nusu-fainali.

Uingereza walikuwa wakipania kutawazwa wafalme wa Euro kwa mara ya kwanza katika historia, na ushindi dhidi ya Italia ungewavunia taji la pili katika soka ya haiba baada ya kunyakua Kombe la Dunia mnamo 1966.

Kipindi cha miaka 53 ambacho Italia walisubiri kutwaa taji la Euro ndicho kirefu zaidi katika historia ya kipute hicho. Mabingwa mara tatu, Uhispania, waliwahi kusubiri kwa miaka 44 kuanzia 1964 hadi 2008 kabla ya kutawazwa wafalme kwa mara ya pili kisha wakaibuka mabingwa kwa mara nyingine mnamo 2012.

Uingereza walimiliki asilimia ndogo zaidi ya mpira (34.4) kwa mara ya kwanza mbele ya mashabiki wao wa nyumbani. Mara ya mwisho kwa kikosi hicho kufanya hivyo ni Novemba 2016 walipolazimishiwa sare ya 2-2 kirafiki kutoka kwa Uhispania.

Wakicheza dhidi ya Italia, Uingereza walipoteza penalti tatu za mwisho zilizochanjwa na chipukizi Bukayo Saka, Marcus Rashford na Jadon Sancho walioletwa uwanjani katika dakika za mwisho kwa kibarua mahsusi cha kupiga matuta.

Tukio hilo lilirejesha taswira ya nuksi ya 1996 ambapo Uingereza walicharazwa 6-5 na Ujerumani kupitia penalti kwenye nusu-fainali za Euro 1996 baada ya kuambulia sare ya 1-1. Gareth Southgate ambaye sasa ni kocha wa Uingereza, alipoteza penalti yake kwenye kipute hicho.

Harry Kane na Harry Maguire ambao ni manahodha wa Tottenham Hotspur na Manchester United mtawalia, walifunga mikwaju yao huku kipa Jordan Pickford akipangua mikwaju ya Andrea Belotti na Jorginho Frello. Wanasoka wa Italia waliofunga penalti zao ni Domenico Berardi, Bonucci na Federico Bernardeschi.

Kabla ya kutinga fainali ya Euro mwaka huu, Uingereza waliwahi kunusia ubingwa wa soka ya haiba kubwa mnamo 2018 ila wakadenguliwa na Croatia kwa kichapo cha 2-1 kwenye nusu-fainali za Kombe la Dunia jijini Moscow, Urusi.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mgombea wa ubunge Kiambaa kwa tiketi ya UDA alia serikali...

Mashindano ya kuogelea sasa kuanza Ijumaa jijini Mombasa