Mashabiki waruhusiwa kuingia viwanja vya Kenya kwa mara ya kwanza tangu Machi 2020

Mashabiki waruhusiwa kuingia viwanja vya Kenya kwa mara ya kwanza tangu Machi 2020

Na VICTOR OTIENO

WAPENZI wa michezo sasa wanaweza kuingia viwanjani kushangilia timu zao baada ya serikali kutangaza kuwa imeondoa marufuku dhidi ya mashabiki.

Kufuatia tangazo la Rais Uhuru Kenyatta siku ya Mashujaa Dei (Oktoba 20) kuwa masharti ya kudhibiti ugonjwa wa Covid-19 yaangaliwe upya, na majadiliano yaliyofuatia kati ya Mawaziri Amina Mohamed (Michezo) na Mutahi Kagwe (Afyia), mashabiki sasa watarejea viwanjani.

Hata hivyo, serikali imewapa waandalizi wa michezo sharti la kuhakikisha kuwa mashabiki hawazidi thuluthi mbili. Kwa mfano, viwanja vya kimataifa vya Kasarani na Nyayo vinavyobeba mashabiki 60,000 na 45,000 mtawalia sasa zitakubaliwa kuwa na mashabiki 40,000 na 30,000 mtawalia.

Mnamo Ijumaa, serikali ilikuwa imekubali idadi ndogo ya mashabiki kuingia ugani Nyayo kutazama mchuano wa marudiano wa Kombe la Mashirikisho kati ya wenyeji Gor Mahia na Ahly Merowe kutoka Sudan zitakapomenyana hapo Oktoba 24.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Afya Patrick Amoth amethibitisha Jumamosi kuwa mashabiki wataruhusiwa viwanjani, lakini kwa kuzingatia masharti ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa Covid-19.

“Sioni tatizo liko wapi mashabiki wakiruhusiwa kuingia viwanjani tena kwa sababu wanasiasa wamekuwa wakifanya mikutano mikubwa kila siku,” alisema Amoth. Katika tovuti yake, Gor Mahia ilisema kuwa Wizara ya Afya na Shirikisho la Soka Kenya (FKF) zimekubali mashabiki 10,000 wafike uwanjani Nyayo hapo Jumapili.

Taarifa ya Amoth hapo Jumamosi inamaanisha kuwa Gor inakubaliwa kuwa na mashabiki hata zaidi. Serikali iliwekea mashabiki marufuku siku chache tu baada ya Kenya kuthibitisha kisa cha kwanza cha corona mnamo Machi 12, 2020.

Gor inaongoza Merowe 3-1 kutoka ushindi wake katika mechi ya mkondo wa kwanza uwanjani New Suez nchini Misri mnamo Oktoba 15.

You can share this post!

Serikali yasitisha mradi wa Benki ya dunia- WB- wa...

Mashabiki waruhusiwa kuingia viwanja vya Kenya kwa mara ya...

T L