Afya na Jamii

Mashaka ya mwanamke anayeugua maradhi yasiyofahamika kwa miaka 14

May 13th, 2024 2 min read

NA OSCAR KAKAI

AKIWA amelala kwenye kitanda chake cha mbao, katika nyumba ya nyasi ya msonge huku ukuta wa nje ukiwa unavuja maji kutoka kwenye paa kijijini Chekeneroi, wadi ya Siyoi, Kaunti ya Pokot Magharibi, Evelyn Cherop ni mnyonge na yuko kwenye maumivu. 

Hali hiyo ya kuhuzunisha, mazingira mabovu, umaskini na ugonjwa usioeleweka umemuacha mnyonge na hawezi kuondoka kwenye boma.

Mama huyo mwenye umri wa miaka 32, sasa amelazwa kitandani nyumbani bila fedha ama matibabu huku familia yake ikiwa katika hali ya uchochole.

Afya yake imekuwa ikodorora kila siku na sasa hawezi kutemba ama kusimama peke yake.

Kulingana na Cherop ambaye ni yatima, hajawahi kuenda katika hospitali nzuri kupata matibabu.

Amekuwa akienda kwenye zanahati na vituo vya afya vya karibu lakini aliambiwa aende kwa hospitali kubwa ili afanyiwe uchunguzi lakini hana uwezo.

Licha ya masaibu pamoja na changamoto hizo, Bi Cherop alifaulu kumaliza masomo yake katika shule ya upili ya St Mary’s, Siyoi ambapo alipata alama ya  C- lakini hali yake umemharibia maisha.

“Nilikuwa nikienda shuleni nikiwa katika hali hii. Mara nyingi nilikosa kuenda shuleni wakati hali ilikuwa mbaya zaidi. Nilikuwa nikiketi njiani wakati ninaenda shuleni nikishindwa kutembea,”anaeleza.

Bi Cherop ambaye yuko katika hali mbaya sasa amepambana na ugonjwa huo kwa miaka 14.

“Ninaomba Wasamaria Wema, viongozi na hata serikali kunisaidia nipate matibabu,” anasema.

Anasema kuwa ugonjwa huo ulianza akiwa Darasa la Saba mwaka wa 2009.

“Hakuna siku nilisoma vyema darasani, nilikuwa nikikosa kuenda shuleni. Nilikuwa nikitembea na mkongojo kuenda shuleni. Nilikuwa ninaumwa lakini sio sana kama sasa na nikaanza kutumia dawa za kutuliza uchungu,” anasema.

Anasema kuwa amekuwa akitumia dawa za kutuliza uchungu kwa miaka yake yote.

“Huwa silali usiku. Sielewi ninaugua kutokana na nini. Nashindwa ni makossa gani nilimfanyia Mungu?” anauliza.

Anasema kuwa yeye hutegemea dadake ambaye hana ajira kumlisha.

“Ninategemea dadangu na wakati anakosa kibarua tunalala tu njaa. Sina baba wala mama,” anasema.

Anasema kuwa amekuwa mzigo kwa watu.

“Familia yangu hunibeba kunitoa nje na kunirudisha ndani ya nyumba. Wengine wamekuwa wagonjwa kifua sababu ya kunibeba na hata wamechoka. Mimi huenda haja penye nipo,” anasema.

Anasema kua dalili za ugonjwa wake ni miguu kufura na kuumwa na misuli mwili wote.

“Fikiria tu kukwama kwenye boma bila uwezo wa kutembea, bila matibabu ama mtu wa kukusaidia. Mimi hulala mchana na usiku nikiuguzwa tu,” anasema.

Kutokana na hali yake anasema kuwa maisha yamekosa maana.

“Nimeumia kutoka utotoni hadi ukubwani. Siwezi kutembea wala kufanya chochote. Mikono zangu haziwezi kunyooka na zimepooza. Sina usaidizi. Sio rahisi kushinda kitandani maisha yangu yote. Sasa nimechoka na maisha,” anasema.

Bi Cherop ambaye ni mama wa mtoto mmoja anaomba usaidizi.