Habari Mseto

Mashambulio mapya bondeni yazima juhudi za amani

April 4th, 2019 1 min read

BARNABAS BII na WYCLIFF KIPSANG

MASHAMBULIO yamezuka upya miongoni mwa jamii za wafugaji katika eneo la Kaskazini mwa Rift Valley, huku watu zaidi ya 10 wakiwa tayari wameuawa na wengine kuachwa bila makao.

Mapigano hayo mapya ni changamoto katika juhudi za serikali na viongozi wa eneo hilo kutafuta amani ya kudumu.

Hali ya taharuki imegubika Kaunti za Elgeyo Marakwet na Baringo baada ya wanafunzi wawili kuuawa na wengine kujeruhiwa katika shambulio la kulipiza kisasi lililotokea katika eneo la Endo.

Mapigano hayo baina ya wafugaji wa kuhamahama wa jamii ya Wamarakwet na Wapokot ni pigo kwa juhudi za kutaka kuhakikisha kuwa jamii hizo zinaishi kwa amani.

Kamishna wa Ukanda wa Bonde la Ufa, Mongo Chimwaga alithibitisha kuwepo kwa mashambulio hayo huku akisema kuwa maafisa zaidi wa usalama wametumwa katika eneo hilo.

“Tumeanza kuwashirikisha wazee kutoka kaunti za Pokot Magharibi, Turkana, Baringo na Elgeyo Marakwet katika juhudi za serikali kutaka kumaliza uhasama baina ya jamii hizo mbili,” akasema Bw Chimwaga.

Alisema ukame unaoendelea kushuhudiwa katika eneo hilo umesababisha ukosefu wa maji na malisho hivyo kuzua uhasama miongoni mwa jamii za wafugaji wa kuhamahama.

“Serikali imeongeza idadi ya maafisa wa usalama na hata kuboresha vyanzo vya maji kwa lengo la kuzuia mapigano,” akasema Bw Chimwaga.

Pia alisema kuwa polisi wa akiba (NPR) watafanyiwa usajili upya.

“Polisi wa akiba watasajiliwa upya ili kuwezesha serikali kujua idadi yao na bunduki walizo nazo na kuwawezesha kukabiliana na wahalifu,” akasema.

Alisema mbuzi 45 waliibwa wakati wa shambulio la Jumanne katika eneo la Kainuk katika mpaka wa Pokot Magharibi na Turkana.

“Mashambulio hayo yameathiri pakubwa shughuli za kiuchumi miongoni mwa jamii za kuhamahama na hali itakuwa mbaya zaidi iwapo hakutakuwa na suluhu la kudumu,” akasema.