Kimataifa

Mashambulizi dhidi ya raia wa kigeni Afrika Kusini yaushtua ulimwengu

September 3rd, 2019 2 min read

Na AFP na MARY WANGARI

JOHANNESBURG, Afrika Kusini

WAZIRI Mkuu David Makhura amesema mashambulizi ya ubaguzi wa rangi hayataruhusiwa Gauteng, Afrika Kusini na kuitisha utulivu katika maeneo yaliyoathiriwa huku polisi wakiimarisha doria kufuatia visa vya ghasia na uporaji.

Matamshi yake yalijiri huku Serikali ya Nigeria ikitaja mashambulizi hayo kama yasiyofaa ambapo Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amepanga kukutana na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa mnamo Oktoba kuhusiana na kuongezeka kwa mashambulizi hayo.

Hata hivyo, Makhura alisema hataomba msamaha kwa raia wa kigeni wanaoshiriki uhalifu, akidokeza kwamba kufikia sasa, polisi wanaendelea kupambana visa vya uporaji na uhalifu mkoani humo na kwamba hali ilikuwa shwari.

“Hatuwezi kuwachukulia raia wote wa kigeni kama wahalifu na wale wanaohusika katika uhalifu ni sharti wakabiliwe. Kila mtu ni sharti atii sheria awe raia wa taifa hili au wa raia wa kigeni, “alisema Makhura.

Alisema vitendo vya uporaji haviwezi kutetewa kwa ukosefu wa ajira na visa vya uhalifu akisema hatafidia wamiliki wote wa duka ambao wamepoteza mali yao.

Kulingana na Makhura, Afrika Kusini inakabiliana na raia wa kigeni haramu ambao hawajasajiliwa huku akiahidi kuimarishwa kwa usalama mipakani kuhakikisha eneo hilo lina utulivu.

Kiongozi wa Economic Freedom Fighters (EFF) Julius Malema, alitoa hakikisho kwamba Afrika Kusini ni ya watu wote huku akilaani kuzuka kwa mashambulizi ya ubaguzi wa rangi dhidi ya raia wa kigeni nchini humo.

Rais wa Muungano wa Nigeria Afrika Kusini (NUSA), Adetola Olubajo aliyethibitisha maendeleo hayo kwa vyombo vya habari alisema mashambulizi hayo yalianza mnamo Jumapili asubuhi eneo la Jeppestown mjini Johannesburg wakati jumba liliteketezwa na umati uliojawa na ghadhabu.

Malema alitoa wito wa kukomesha mashambulizi hayo dhidi ya raia wa kigeni akisema Afrika Kusini ni ya watu wote.

Katika taarifa aliyotia sahihi, Malema pia alipuuzilia mbali madai kwamba raia wa kigeni walikuwa wakichukua kazi zinazostahili kupatiwa wananchi wa Afrika Kusini.

“Uwe umetoka Afrika Kusini, au umetoka Zimbabwe, ama umetoka Nigeria, hapa ni nyumbani kwako. “Hakuna ajira katika taifa la Afrika Kusini kwa sababu Wamagharibi wanakataa kuwekeza fedha Afrika Kusini, wana akiba nyingi mno kwenye benki.

“Wakati ni mzungu nchini Afrika Kusini ambaye hajasajilishwa anaitwa mwekezaji, ikiwemo raia wa India na Uchina.

Lazima kujichukia sisi wenyewe kukome!” “Afrika sisi ni wamoja. Raia wa Nigeria ni kaka zetu. Acha tuvumiliane.”