Michezo

Masharti 6 aliyotaka Zidane kabla ya kukubali kuinoa Real tena

March 12th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

SIKU moja tu baada ya Zinedine Zidane kukubali kurejelea kazi ya ukufunzi katika timu ya Real Madrid, imefichuka kwamba alitoa masharti sita mazito kabla ya kuchukua kazi hiyo kwa uongozi wa timu hiyo.

Nyota huyo wa zamani wa Real Madrid na timu ya Taifa ya Ufaransa maarufu kama The Les Blues, alijiuzulu kama kocha wa Los Blancos miezi 12 iliyopita japo Jumatatu Machi 11, alirejea na kumwaga wino kwenye kandarasi itakayomweka ugani Santiago Bernebeu hadi mwaka wa 2022.

Rais wa Real Madrid Florentina Perez anadaiwa kuridhia masharti hayo ya Zidane ambaye alishinda Kombe la Dunia kama mchezaji mwaka wa 1998. Zidane aliondoka Real baada ya kushinda mataji matatu ya Klabu Bingwa Barani Uropa miaka mitatu ikifuatana.

Masharti hayo yalikuwa:

  1. Kuchukua usimamizi kikamilifu wa timu
  2. Kuwapiga bei wachezaji asiowataka
  3. Kutowauza wachezaji Marcelo na Isco
  4. Kutonunua nyota wa PSG Neymar
  5. Kutomruhusu mshambulizi James Rodrigez anayeisakatia Bayern Munich kwa mkopo kurudi Real Madrid, na
  6. Kumsajili Kylan Mbappe kutoka PSG.

Real Madrid waliagana na aliyekuwa kocha wao Santiago Solari kutokana na misururu ya matokeo mabaya.