Habari

Masharti haya ni kwa ajili ya afya zenu, waziri aambia Wakenya

March 20th, 2020 1 min read

Na SAMMY WAWERU

SERIKALI imetoa masharti na tahadhari muhimu kuzingatiwa kukabili maenezi ya Covid-19.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe ametoa tahadhari kwa taifa akiwataka wananchi watarajie kupitia kipindi kigumu, lakini akisema ni hatua muhimu kwa ajili ya kuhakikisha wanakuwa na afya bora.

Akihutubu Ijumaa jijini Nairobi katika Afya House, waziri huyo amesema hakuna kampuni, shirika au biashara ambayo haijaathiriwa kwa njia moja au nyingine kutokana na kuripotiwa kwa visa kadhaa vya maambukizi ya virusi hivyo hatari vya corona.

Kufikia sasa Kenya imethibitisha kuwa na visa saba vya watu walioambukizwa.

Hata ingawa hajataja kuongezeka kwa visa vingine, Bw Kagwe amekiri kuwa serikali inapitia magumu hasa katika operesheni nzima kuzuia maambukizi zaidi, ikizingatiwa kuwa Kenya haijawahi kushuhudia janga kama la Covid-19.

Serikali imeagiza maeneo yote ya burudani, baa zikiwemo, kuanza kufungwa saa moja na nusu usiku.

“Agizo linaanza kutekelezwa Jumatatu, Machi 23, 2020,” amesema waziri Kagwe.

Licha ya shinikizo serikali ihakikishe imenusuru uchumi ili raia wake wasihangaike, waziri amesema muhimu zaidi ni kuyapa maisha ya wananchi kipaumbele.

“Tunaweza kunusuru uchumi, lakini la msingi na muhimu zaidi ni kuokoa maisha ya kila Mkenya,” akasisitiza, akionekana kulenga utaratibu na maagizo yaliyotolewa na serikali.

Aidha, kila mtu anatakiwa kudumisha kiwango cha hadhi ya juu cha usafi, na kuepuka kushiriki mikutano.

Ili kuzuia maenezi zaidi ya Covid-19, mapema wiki hii serikali ilitangaza kupiga marufuku mikutano ya hadhara.

Watu wanatakiwa kutilia maanani kigezo cha umbali wa mita moja au zaidi wanapotangamana.

Serikali pia imeamuru idadi ya abiria wanaobebwa mara moja kwa matatu ishushwe, mfano matatu ya abiria 14 ibebe 8, ikionya kwamba wamiliki na wahudumu watakaokaidi amri hiyo watachukuliwa hatua kali kisheria.

Inakisiwa kwa muda wa wiki mbili zajazo, Kenya huenda ikapitia nyakati ngumu, kulingana na hali inayoshuhudiwa katika mataifa yaliyotajwa kuathirika pakubwa na janga la Covid-19.

Tayari wananchi na wafanyabiashara wameanza kulalamikia maisha magumu, biashara nazo zikianza kufifia.