Makala

Masharti magumu ya wavuvi kushusha nyavu baharini

February 21st, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

UKIWA mvuvi halisi kwenye baadhi ya maeneo ya mwambao wa Pwani, hasa Lamu, itakujuzu kuzingatia kikamilifu baadhi ya miiko au masharti ili kudumu kwenye sekta hiyo.

Kuna wavuvi wengine, hasa wa kizazi cha sasa, ambao wamekuwa wakiyasuta masharti au marufuku hayo kwa kuyaona kuwa utumwa, ushirikina au imani zilizopitwa na wakati.

Cha kushangaza ni kwamba licha ya kejeli zao, wavuvi hao wa kisasa mwisho wa siku pia huishia kuheshimu hayo masharti wayaonayo kuwa ‘zilipendwa’.

Miongoni mwa masharti hayo ni mvuvi kutoingia baharini wakati akiwa amejistarehesha na mkewe au mchumba wake na kisha kukosa kuoga janaba.

Mvuvi mkongwe na Mwenyekiti wa Miungano ya Wavuvi (BMUs) katika kaunti ya Lamu Mohamed Somo, anasema ni jukumu la kila mvuvi kuhakikisha anajisafisha ipasavyo kabla ya kujumuika na wenzake kuenda baharini, akidai kuwa kukaidi hilo ni sawa na kujiletea mikosi.

Mwenyekiti wa wavuvi wa Lamu, Mohamed Somo. Anasema ili kuepuka mikosi au visirani baharini, lazima wavuvi wawe wasafi wa mwili, hasa kwa wale wanaolala na wake zao au wachumba na kisha kuchomoka kuingia baharini bila kuoga janaba. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Somo anasema walizaliwa na kuyakuta masharti hayo yakiheshimiwa na wazazi wao, hivyo na wao kuyarithi hadi leo.

Inaaminika kukaidi miiko kama hiyo humletea mvuvi nuksi si haba, ikiwemo chombo kuzama baharini katika hali isiyoeleweka, migogoro kuzuka kati ya wavuvi husika na kukosa kabisa pato la siku au la usiku la samaki, hivyo kurudi nyumbani mikono mitupu.

“Mababu na wazazi wetu walitii miiko hii ya wavuvi kukoma kuenda baharini baada ya starehe na mke na kisha kudamka na kukimbilia baharini kuvua samaki bila kuoga janaba. Ukifanya hivyo ni kujiletea mikosi kwanza kwako wewe binafsi na pia kwa wale wenzako mnaoshirikiana kuenda baharini kwa shughuli za uvuvi. Miongoni mwa nuksi mbaya zaidi zinazoaminika kuletwa na imani hizo ni mashua kuzama na hata wavuvi kufariki,” akasema Bw Somo.

Bw Ali Bashali, ambaye amekuwa mvuvi kisiwani Lamu kwa zaidi ya miaka 20, anasema yeye binafsi kwa wakati mmoja amejipata kwenye tatizo hilo.

Bw Bashali aidha anasema alijitambua mapema na kuwaeleza wenzake walipokuwa katikati ya bahari kilichokuwa kimetendeka, hivyo akasaidiwa na wenzake kuruka baharini kuogelea kwa muda na kisha kurudi kwenye mashua kuendelea na shughuli za siku hiyo.

Ali Bashali, mvuvi wa Lamu kwa zaidi ya miaka 20. Anasema ni vyema miiko iliyopo miongoni mwa wavuvi iheshimiwa kwani ipo siku alijipata mashakani baada ya kwenda kinyume na masharti hayo. PICHA | KALUME KAZUNGU

“Hii imani ni ya kweli kabisa. Ipo siku niliruka kitandani na kukimbilia ufuoni kushikana na wavuvi wenzangu kuenda baharini kuvua samaki. Nilikuwa nimechelewa. Tulikuwa wavuvi 10 na tulipofika katikati ya bahari chombo chetu kikaanza kwenda mrama. Hapo sikusubiri. Nilieleza wenzangu kwamba sikuwa nimeoga janaba. Hapo walinirusha mara moja baharini kuogelea na kisha kurudi mashuani. Cha kustaajabisha ni kwamba bahari ilitulia na mambo yakawa shwari kabisa,”  akasema Bw Bashali.

Masharti mengine ambayo wavuvi wa Lamu na hata mabaharia pia wametii, hivyo kuwawezesha kudumu kwenye shughuli zao za kila siku na kuepuka visirani ni mja kwenda haja ndogo ndani ya boti, hasa kwa upande wa mbele.

Ahmed Athman anasema kufanya hivyo ni sawa na kukitia kisirani chombo husika cha usafiri.

“Mvuvi au baharia yoyote hafai kujisaidia haja ndogo akiwa amesimama mbele ya boti au mashua. Punde unapofanya hivyo safari haitakamilika. Kuna uwezekano mtapata ajali au kutokee pingamizi nyingine itakayowafanya kukatiza safari yenu ya kwenda kuvua baharini siku hiyo,” akasema Bw Athman.

Bakari Vae, mvuvi wa Kizingitini, anasema uaminifu pia ni jambo muhimu kwa mvuvi wa Lamu.

Mmojawapo wa wavuvi akibeba samaki mkubwa kumpeleka kwa hifadhi ya barafu kisiwani Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Anasema endapo wavuvi watakosa kuaminiana kwa kila jambo, hilo pekee pia huwaletea kisirani.

Bw Vae anasisitiza kuwa kama mvuvi, hasa ambaye unashirikiana na wenzako, hufai kuiba kisiri samaki mnaovua au kudanganya kiwango cha fedha ambacho kimetokana na kuvua kwenu.

“Ili mfaulu kama wavuvi, lazima muwe na uwazi kati yenu. Punde kunapokuwa na mmoja ambaye ataiba shehena ya samaki na kisha kudanganya wenzake, hiyo tayari ni chanzo cha mikosi. Siku nyingine mkienda baharini mtaishia kugombana na kurudi nyumbani mikono mitupu. Lazima wavuvi wawe wenye kushirikiana na kudumisha uwazi na uwajibikaji,” akasema Bw Vae.

Lamu ina zaidi ya wavuvi 7,000 wapatikanao kwenye zaidi ya visiwa 35 vya eneo hilo.

Miongoni mwa ngome kuu za uvuvi Lamu ni Kiunga na Ishakani zilizoko mpakani mwa Kenya na Somalia, Kizingitini, Faza, Ndau, Kiwayu, Mkokoni, Zinyika, Pate, Siyu, Mtangawanda, Lamu mjini, Shella, Matondoni, na Kipungani.