Habari Mseto

Masharti makali kwa wote wanaotaka kuwa walinzi

February 24th, 2019 2 min read

Na ELVIS ONDIEKI

SERIKALI imetoa masharti mapya makali kwa watu wanaotaka kujiunga na kampuni za walinzi wa kibinafsi katika juhudi za kuimarisha utendakazi wao.

Sasa, watu wote wanaotaka kuwa walinzi wa kibinafsi almaarufu ‘askari rungu’ nchini watakuwa wakipata mafunzo ya kazi hiyo kwa saa 240 ambayo ni muda wa mwezi moja kabla ya serikali kuwaruhusu kuajiriwa. Wafanyakazi wengi huhitajika kufanya kazi kwa muda usiozidi saa nane kwa siku, na katika masharti haya mapya, walinzi hao watapata mafunzo kwa mwezi huku wakichukua 20 kujifahamisha na kazi yenyewe.

Walinzi wanaohudumu kwa sasa watakuwa wakipata mafunzo kwa saa 40 au siku tano kabla ya kuruhusiwa kuendelea kuhudumu. Masharti haya, yapo kwa mtaala wa mafunzo ya walinzi wa kibinafsi ambao Taifa Jumapili imefaulu kuupekua.

Mtaala huu unalenga kuhakikisha kwamba walinzi wote wa kibinafsi watakuwa wakipata mafunzo sawa na umeandaliwa na Mamlaka ya Walinzi wa Kibinafsi ya Kenya.

Mtaala huo unatilia mkazo huduma ya kwanza ambapo walinzi wapya watakuwa wakitumia muda wa saa 12 kufunzwa na wale wanaohudumu saa watafunzwa huduma hiyo kwa saa sita.

Walinzi hao pia watakuwa wakipata mafunzo kuhusu kukabiliana na ugaidi ambayo yatawachukua walinzi wapya saa sita.

“Masomo pia yatahusu kutambua makundi ya kigaidi ambao hulenga kuua Wakenya wasio na hatia kwa kutumia vilipuzi, silaha na mbinu nyingine hatari,” unaeleza mtaala huo.

“Baada ya kukamilisha mafunzo, mwanafunzi atakuwa na uwezo mzuri wa kuelewa ugaidi katika ulimwengu wa sasa,” wanaeleza waandalizi wa mtaala huo.

Walinzi hao pia watakuwa wakifunzwa jinsi ya kuandika ripoti, kudumisha maadili na kujiandaa kukabiliana na dharura. Baada ya mafunzo ambayo waandalizi wa mtaala wanasema ni lazima yafanyiwe kwenye darasa, walinzi hao watakuwa wakifanya mtihani.

“Ni wanafunzi waliohudhuria mafunzo yote darasani ambao watafunzu kufanya mtihani,” zinaeleza kanuni mpya za kuthibiti sekta ya ulinzi wa kibinafsi.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Walinzi wa Kibinafsi Bw Fazul Mahamed, alisema mtaala huo utabadilisha sekta ya ulinzi nchini.

“Mtaala huo utawapa walinzi uwezo wa kutambua, kuzuia na kukabiliana kikamilifu na vitisho katika karne ya ishirini na moja,” Bw Fazul aliambia Taifa Jumapili.

“Huu ni mwelekeo unaohusisha serikali katika sekta ya walinzi wa kibinafsi,” aliongeza Bw Mahamed.

Mnamo Desemba, Bw Fazul aliambia wadau katika sekta ya ulinzi wa kibinafsi kwamba mafunzo yataendeshwa kwa ushirikiano wa taasisi za mafunzo anuwai na Mamlaka ya Taifa ya kutoa mafunzo ya kiufundi.

Bw Fazul aliongeza kuwa baada ya kupata mafunzo, walinzi hao watakuwa wakikaguliwa kabla ya kukabidhiwa leseni. Ni walio na leseni hizi ambao watakuwa wakipatiwa silaha wakiwa kazini.