Masharti makali ya kutoshiriki ngono waliopona Ebola

Masharti makali ya kutoshiriki ngono waliopona Ebola

NA DAILY MONITOR

KAMPALA, UGANDA

WATU waliopona Ebola wametakiwa kusubiri hadi baada ya miezi mitatu kabla ya kushiriki ngono au watumie kondomu ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo, Wizara ya Afya nchini Uganda imeshauri.

“Kabla ya kurejea nyumbani, wagonjwa wa Ebola watafanyiwa vipimo vya damu katika maabara kuthibitisha kuwa hawana virusi vinavyosababisha ugonjwa huu.

“Hata hivyo, watu waliopona kutokana na Ebola sharti waepukane na ngono kwa angalau miezi mitatu. Ikiwa watataka kushiriki tendo hilo, basi sharti watumie mipira ya kondomu,” ikaeleza wizara hiyo kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi kuhusu Virusi Uganda (UVRI), Profesa Pontiano Kaleebu, alisema ingawa Ebola inachukuliwa kama ugonjwa usioenezwa kupitia ngono, baadhi ya wataalamu wamepata virusi vyake katika mbegu za kiume au shahawa (Kimombo semen) ya wanaume waliopona.

Naye Dkt Ataro Ayella – mtaalamu ambaye ameshughulikia mikurupuko ya Ebola katika mataifa ya Afrika Magharibi – alisema ugonjwa huo unaweza kusambazwa kupitia ngono.

Dkt Ayella alishiriki katika kampeni za kudhibiti Ebola nchini Liberia mnamo 2017 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) mnamo 2019.

“Virusi vinavyosababisha Ebola husalia katika mbegu za kiume hadi miezi mitatu. Inamaana kuwa maambukizi yanaweza kufanyika hata kama aliyepona haonyeshi dalili zozote za ugonjwa,” mtaalamu huyo alisema kwenye mahojiano jana Ijumaa.

Dkt Ayella aliongeza kuwa watu waliopona Ebola wanaweza kupata maambukizi mapya baada ya muda.

“Hata hivyo, hali hii hutegemea kinga ya mwili wa mhusika au kuwepo kwa ugonjwa mwingine tofauti mwilini,” akaongeza.

Wanasayansi wanasema tafiti zilizofanywa nchini Liberia zilipata kuwa, mwanamke mmoja aliambukizwa Ebola baada ya kushiriki mapenzi na mwanamume aliyekuwa amepona ugonjwa huo.

Dkt Charles Olaro, ambaye ni mkurugenzi wa huduma za magonjwa ya kuambukiza, alisema virusi vya Ebola hujificha katika ndani ya korodani baada ya mgonjwa kupona.

Alipoulizwa wakati ambapo kipindi cha miezi mitatu cha kuasi ngono huanza kuhesabiwa, Dkt Olaro alisema, “kuanzia siku ambayo manusura ameruhusiwa kuondoka hospitalini.”

Dkt Ayella anaeleza kuwa virusi vinavyosababisha Ebola pia vinaweza kujificha katika sehemu zingine kama vile uti wa mgongo na machoni mwa manusura.

“Maumbile ya virusi vya Ebola yanaipa uwezo wa kuishi kwa muda mrefu kwenye ubongo, uti wa mgongo, mbegu za kiume, nyumba ya uzazi na kwenye macho, hata baada ya mgonjwa kuthibitishwa kuwa amepona. Virusi hivyo vinaweza kuishi katika mbegu za kiume kwa muda mrefu kuliko majimaji ya mwili,” Dkt Ayella anaeleza.

Watu wengi waliozungumza na Daily Monitor walitoa wito kwa serikali ya Uganda kuendeleza uhamasisho kuhusu ugonjwa huo.

Bi Grace Aine, ambaye ni mfanyabiashara mjini Kampala alisema: “Wizara ya Afya inafaa kutoa uhamasisho kwa raia. Nina uhakika kwamba sio kila mtu anafahamu kuhusu ugonjwa huu ilhali idadi ya maambukizi inaendelea kupanda kila mara.”

“Nina imani kwamba watu watatii ikiwa watafahamu athari zake. Ni vizuri kwamba wanasema ni sawa kwa mtu kuvalia kinga kabla ya kushiriki ngono,” akaongeza.

Bw Alex Ariho, mkazi wa Kampala naye akasema; “Ujumbe huu unafaa kuwafiki watu wote wanaouhitaji, haswa makahaba. Wasisitize kuwa sharti wajikinge wanapoendesha biashara hii.”

  • Tags

You can share this post!

Korti yaamua wajane wana haki kurithi mali wakiolewa tena

Achani azindua kampeni dhidi ya Ukimwi

T L