Habari za Kitaifa

Masharti makali yawekwa kwa wanaonuia kufanya KCSE/KPSEA ya 2024

January 8th, 2024 1 min read

Na BENSON MATHEKA

Walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari wamepatiwa masharti makali ya kusajili watahiniwa wa mitihani ya Gredi ya sita (KPSEA) na Kidato cha Nne (KCSE) ya mwaka huu.

Usajili huo utaanza  Januari 29 hadi Machi 29 bila kuchelewa na muda huo hautaongezwa ilivyokuwa miaka iliyopita.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Baraza la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNEC) Dkt David Njengere alitangaza kuwa baada ya kipindi hicho na miezi miwili, usajili utafungwa.

Akihutubu katika hafla ya kutoa matokeo ya mtihani wa KCSE wa mwaka jana katika Shule ya Wasichana ya Moi Girls Kaunti ya Uasin Gishu, Dkt Njengere alisema kwamba muda huo hautaongezwa.

“Hiki ni kipindi cha miezi 2 ambacho kinatosha kwa shule kusajili na kuthibitisha data ili kuhakikisha kwamba maelezo yote ya watahiniwa yanapakiwa kwenye mtandao wa usajili na kwamba data ni sahihi,” alisema Dkt Njengere.

Aliwaagiza wasimamizi wa vituo vya mitihani kuhakikisha kuwa habari zote za watahiniwa ni sahihi akisema watahiniwa ambao hawatakuwa katika hifadhidata ya usajili mwishoni mwa kipindi cha usajili hawatakuwa na karatasi za mitihani mwishoni mwa mwaka.

Walimu wakuu wa shule ndio wasimamizi wa vituo vya mitihani na ndio husajili watahiniwa.

“Hakutakuwa na nafasi ya kubadilisha picha baada ya usajili kufungwa. Wasimamizi wa vituo watawajibikia watahiniwa hewa na hivyo basi watatarajiwa kuwajibika kwa watahiniwa wote ambao hawatakuwa wamesajiliwa,” akaeleza.

Dkt Njengere aliwahimiza wazazi na walezi kuhakikisha kuwa watoto wao watakuwa na stakabadhi muhimu kwa mchakato wa usajili.

Kumekuwa na visa vya wanafunzi kugundua hawakusajiliwa kufanya mitihani ya kitaifa dakika ya mwisho.

Dkt Njengere alihimiza wazazi kuchukua hatua na kuthibitisha kwamba watoto wao watakuwa wamesajiliwa ndani ya muda wa miezi miwili ambao KNEC imetoa kwa zoezi hilo.