MASHEMEJI: AFC Leopards kualika Gor Mahia ugani Nyayo mnamo Jumapili

MASHEMEJI: AFC Leopards kualika Gor Mahia ugani Nyayo mnamo Jumapili

NA JOHN ASHIHUNDU

BAADA ya muda mrefu tangu msimu uliopita umalizike mwaka 2022, mashabiki wa soka nchini watapata fursa ya kushuhudia mechi kubwa kati ya AFC Leopards na Gor Mahia ambayo ni moja kati ya debi kubwa barani Afrika.

Wakati mashabiki wakiendelea kutambiana mitandaoni, wachezaji wa timu hizi mbili wanaendelea kujinoa vilivyo kwa mechi hiyo itakayochezewa Nyayo Stadium, Jumapili, kuanzia saa tisa.

Hii itakuwa mara ya 95 baada ya timu hizo kukutana mara ya mwisho mnamo Mei, 2022, na kutoka sare 1-1 ugani MISC, Kasarani.

Leopards walitangulia kuona lango kupitia kwa Victor Omune dakika ya 35 kabla ya Gor Kusawazisha kupitia kwa Benson Omalla, dakika ya 51.

Ni mechi inayobeba hisia za mashabiki wengi hapa nchini na hata nje ya Kenya maarufu kama Mashemeji Derby.

Kwa mashabiki wa Leopards, mambo yamekuwa magumu ikikumbukwa kwamba timu yao haijawahi kushinda Gor Mahia tangu 2016. Isitoshe, Gor Mahia ambao waliundwa mnamo 1968 imeshinda ubingwa wa ligi mara 18, wakati Leopards wanajivunia mara 13.

Hata hivyo, kulingana na utafiti uliofanywa kwa wiki chache zilizopita, kuna uwezeskano wa Leopards kuibuka na ushindi mara hii, baada ya kuandikisha ushindi mara tatu mfululizo wa 2-1, 2-0 na 1-0, dhidi ya Mathare United, Bandari FC na Kenya Police mtawaliwa. Leopards ni timu iliyoanzishwa mnamo 1964 mtaa wa Shauri Moyo na ndio timu kongwe kabisa nchini.

Huku joto la watani hao wa jadi likizidi kupamba moto, kuelekea kwa pambano hilo, Gor Mahia wamecheza mechii tisa na kupata ushindi mara saba, wakati Leopards wakijivunia ushindi mara tano baada ya kujibwaga uwanjani mara 11.

Timu hizi zinakutana baada ya kila moja kuendelea matokeo bora katika mechi za karibuni. Katika kuelekea mechi hii kubwa, maafisa wa polisi wanatarajiwa kuhakikisha kuna usalama wa kutosha kwa mashabiki na wachezaji.

Ni mashabiki 20,000 pekee watakaokubaliwa kuingia uwanjani Jumapili kwa ajili ya pambano hilo katika uwanja Nyayo ambao una uwezo wa kubeba zaidi ya mashabiki 30,000 tangu ufanyiwe ukarabati wa kimataifa.

Mashabiki kadhaa wamekuwa wakifuata mechi kupitia kwa televisheni kutokana na hofu ya usalama, lakini kutokana na hakikisho la polisi na taratibu zilizowekwa kuhakikisha mechi hii imechezwa katika mazingira mazuri, huenda Leopards wakaokota pesa kutokana na malipo ya milangoni.

Kikosi cha K’Ogalo kitapangwa na kocha Johnathan McKinstry kutoka taifa la Ireland Kaskazini, wakati Leopards ikiwa chini ya Patrick Aussems, raia wa Ubelgiji.

  • Tags

You can share this post!

Uhispania wapewa Italia huku Uholanzi wakionana na Croatia...

Afisa wa polisi aagizwa ajisalimishe bila kupoteza hata...

T L