Michezo

Mashindano ya karate yapamba moto mjini Thika

March 13th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO
MASHINDANO ya Karate ya Kenya Opens Championship, yalifanyika wikendi iliyopita katika ukumbi wa Arena Indoors katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya mjini Thika.
Mkufunzi wa timu kuu ya karate nchini Bon Awiti alisema mashindano hayo yalikuwa katika vitengo tofauti vya Kata na Kumite.
Hii ilikuwa ni njia moja ya kupata wachezaji ambao watajiandaa kwa mashindano tofauti yatakayofanyika katika nchi tofauti za Bara Afrika kwa muda wa mwaka huu wa 2019,” alisema Bw Awiti.
Alisema kuna misururu ya mashindano yanayowangojea wachezaji hao ambapo wataendelea na mazoezi yao kwa kibarua hicho.
Baadhi ya mashindano hayo ni yale ya Botswana katika miezi michache ijayo.
Mengine ni ya Afrika Kusini yatambulikayo kama Beach Games.
Mengine ni Zone 5 ANOCA ambayo yanahusisha vijana.
Pia kuna michezo ya Morocco ambayo inakuja hivi karibuni.
Wakati wa majaribio hayo ya Kenya Opens jumla ya wanamichezo 340 walishiriki wakiwa ni wa kutoka kaunti 15.
Baadhi tu ya kaunti zilizoshiriki ni Mombasa, Nairobi, Uasin Gishu, Nakuru, Nyeri, Murang’a, Laikipia, na Embu. Zingine ni Bungoma Kisumu, Kakamega, na Kirinyaga.
Aliahimiza wakufunzi wote hapa nchini kufuata sheria za karate jinsi ipasavyo.
“Kuna wengine wetu badala ya kutafuta ushauri kutoka kwa afisi kuu ya Sports Council, wanaendeleza siasa za kichinichini ambazo haziwezi kusaidia yeyote,” alisema Kocha Awiti.
Alisema ili kufanikisha mchezo wa Karate hapa nchini panastahili kuwapo na ushirikiano wa pamoja badala ya kuzungumza mambo ambayo hayamfaidi mwanakarate.
Wakati wa mashindano hayo wanakarate wengi chipukizi walionyesha umahiri wao kwa kurusha mateke kwa njia ya ustadi mkubwa.
“Wanakarate wengi wakiendelea hivyo bila shaka watajenga ujuzi wao na kupiga hatua kubwa katika siku zijazo,” alisema Kocha Awiti.
Alitaka Wizara ya Michezo iliyopewa Bi Amina Mohamed kufanya hima kuona ya kwamba mchezo wa karate inapiga hatua hadi kiwango cha juu zaidi.
“Wakati huu tunataka kuona wizara ya michezo inchukua mstari wa mbele. Sasa ni wakati wa michezo yote nchini kuinuliwa pakubwa. Tusiingize siasa,” alisema kocha Awiti.