Makala

Mashindano ya mbwa yanoga eneo la Diani

March 20th, 2024 2 min read

NA SIAGO CECE

ILIKUWA ni shamrashamra katika maonyesho na mashindano ya mbwa Diani huku mamia ya wakazi na mbwa wao wakijitokeza kwa hafla hiyo katika Kaunti ya Kwale.

Tukio hilo la sita la mashindano ya kila mwaka lililenga kukusanya fedha za kuwalinda wanyama wa kufugwa nyumbani.

Mashindano hayo yalikuwa ya mbwa ambao walishindana katika vitengo kadhaa kikiwemo kile cha kunyaka na kula soseji, kisha mbwa mshindi kutunukiwa.

Kuanzia mbwa waliookolewa, mbwa waliovalia nguo hadi mbwa wakubwa zaidi, hafla hiyo ilileta pamoja zaidi ya washiriki 300 na mbwa 50 wakiwania zawadi mbalimbali.

“Nilimleta mbwa wangu Lucy kwenye onyesho ili kushiriki katika kitengo cha mbwa waliookolewa. Nilimpata kichakani mwaka mmoja uliopita, na nimekuwa nikimlea. Sasa ni rafiki mkubwa wa watoto wangu,” alisema Olivia Mutuku, mkazi.

Bi Olivia Mutuku akiwa na mbwa wake kwa jina ‘Lucy’ wakati wa maonyesho ya mbwa Diani, Kaunti ya Kwale. Bi Mutuku alisema alimwokoa mbwa huyo kutoka kichakani na kumtunza kwa mwaka mmoja. PICHA | SIAGO CECE

Hafla hiyo ya kila mwaka iliyofanyika katika Hoteli ya Safari Beach huko Diani, ilivutia wakazi na watalii kutoka tabaka mbalimbali, huku mbwa walioshinda wakipewa alama na majaji na kutunukiwa katika vipengele mbalimbali ikiwa ni pamoja na mlaji bora wa soseji.

Bi Pauline Mackenzie, ambaye aliandaa maonyesho hayo, alisema mbwa watatu kati ya waliofuzu mchujo ndio walizawadiwa kwa pesa taslimu, madoli na chakula cha mbwa.

“Katika kitengo cha mlaji bora wa soseji, mbwa huingia jukwaani, kisha soseji hutupwa kwao moja kwa moja, asiyekosa ndiye mshindi mwishoni, huku wengine wakikabiliwa na kuondolewa kwenye mchezo,” Bi Mackenzie alisema.

Vitengo vingine ni vya mbwa bora zaidi, wa kike na wa kiume bora, alievalia vizuri zaidi, wa kike na wakiume mkubwa bora na mwenye manyoya bora.

“Tunapanga kila mwaka kuchangisha fedha kwa ajili ya Jumuiya ya Kenya ya Kulinda na Kutunza Wanyama (KSPCA). Wanasaidia sana kuhakikisha kwamba wanyama wengi wanalindwa,” akasema Bi Mackenzie, ambaye pia ni mwakilishi wa KSPCA wa Pwani Kusini.

Wakazi na watalii walipohudhuria maonyesho na mashindano ya mbwa Diani. Washindi walipokea zawadi za pesa, na chakula cha mbwa. PICHA | SIAGO CECE

Mkurugenzi wa Mpango wa KCPCA Mombasa Rachel Griffith alisema moja ya malengo ya onyesho hilo ni kutafuta pesa kusaidia kuokoa maisha ya mbwa.

“Tunatafuta wanyama wanaohitaji usaidizi kutoka kwa jamii na tuwaokoe,” Bi Griffith akasema.

Wakati huo huo, aliipongeza Kenya kwa kuongoza katika haki za ulinzi wa wanyama wa kufugwa barani Afrika, akisema Kenya ina sheria zinazolinda wanyama na mara nyingi kesi za uhalifu dhidi ya wanyama hufikishwa mahakamani.

“Kuna ushirikiano wa ajabu nchini Kenya na kuna watu wengi ambao wanapenda wanyama. Hii ina maana kwamba nchi ina mustakabali mzuri wa ustawi wa wanyama,” alisema Bi Griffins.

Kulingana naye, Wakenya wanaweza kununua na kuwatunza mbwa waliookolewa kutoka kwa ada ya kati ya Sh5,000 hadi Sh9,000 kulingana na ukubwa na aina ya mbwa.

Washindi katika kitengo cha mbwa wadogo zaidi, kabla ya kutuzwa vyeti na mratibu wa shirika la KSCPA Rachael Griffith. PICHA | SIAGO CECE