Habari Mseto

Mashine mpya inayoharakisha 'hesabu' ya virusi vya HIV yazinduliwa

July 16th, 2018 1 min read

Na Elizabeth Ojina

WAATHIRIWA zaidi ya 500,000 wa virusi vya HIV katika maeneo ya Magharibi mwa Kenya sasa huenda wakapata afueni kufuatia uzinduzi wa mashine mpya inayofupisha muda wa kungojea matokeo kuhusu idadi ya viini mwilini.

Mashine hiyo inayojulikana kama Cobas 8800 imewekwa na Taasisi ya Utafiti wa Dawa nchini (Kemri) kwa ushirikiano na Kituo cha Kutafiti Matibabu cha Amerika (CDC).

Mashine hiyo inayotambua idadi ya virusi vinavyosababisha Ukimwi na viini vya maradhi ya malaria mwilini, ilifanyiwa majaribio kwa mara ya kwanza katika Kaunti ya Kisumu miaka miwili iliyopita.

Tangu wakati huo, mashine hiyo imeweza kupima idadi ya virusi katika jumla ya sampuli 500,000 ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 53.

Kulingana na Mkurugenzi wa Utafiti wa HIV katika Mahabara ya KEMRI/CDC Maxwell Majiwa, mashine hiyo inahesabu idadi ya virusi kwenye damu kwa haraka zaidi ikilinganishwa na mashine nyinginezo zilizokuwa zikitumiwa hapo awali.

“Mtambo huu unaongeza kasi ya kupima kiwango cha virusi vya HIV katika sampuli ya damu. Kwa sasa tunaweza kupima sampuli 960 kila baada ya saa nane,” akasema.

Kufahamu idadi ya virusi mwilini kunawezesha madaktari kufahamu aina ya dawa ambayo mgonjwa anastahili kutumia ili kupunguza makali.

Kulingana na ripoti ya wizara ya Afya, kaunti zilizo karibu na Ziwa Victoria katika ukanda wa Nyanza, zinaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya waathiriwa wa virusi vya Ukimwi.

Ukanda wa Magharibi mwa Kenya pia unaongoza katika maambukizi ya malaria.