ZARAA: Mashine za kisasa kuifanya kazi ya upanzi wa mboga iwe rahisi

ZARAA: Mashine za kisasa kuifanya kazi ya upanzi wa mboga iwe rahisi

NA SAMMY WAWERU

WADAU katika sekta ya kilimo, Wanasayansi na watafiti wamekuwa wakihimiza haja ya wakulima kukumbatia mifumo ya kisasa kuendeleza zaraa.

Mifumo hiyo inajumuisha teknolojia za kileo, mitambo, mashine na vifaa.

Bayoteknolojia ni kati ya mifumo hiyo, ambao unajumumuisha bunifu, ikiwemo kuongeza jeni, kuboresha mimea na mifugo ili kupata spishi zilizoboreka kusaidia kupambana na kero ya wadudu na magonjwa.

Hali kadhalika, mfumo wa Bayoteknolojia unasaidia kuafikia usalama wa mazao kwa kupunguza matumizi ya kemikali.

Kando na manufaa hayo, unapunguza gharama katika uzalishaji wa mazao na chakula.

Katika utandawazi huohuo, mashine zinachangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha uzalishaji wa chakula.

Maonyesho ya Kimataifa ya Agritech Africa 2022, yaliyofanyika katika ukumbi wa KICC jijini Nairobi, wakulima na wafugaji kutoka dira tofauti za nchi walipata fursa ya kipekee kutangamana na waonyeshaji hasa kutoka mataifa ya kigeni yaliyoboresha sekta ya kilimo.

Kuna mabarobaro hawa wawili kutoka India, John George na Jaya Guru ambao jukwaa lao lilivutia waliojitokeza wakiwa na hamu kukata kiu cha changamoto za shughuli za kilimo wanazoendeleza.

India ni miongoni mwa nchi zinazofahamika ulimwenguni kuboresha kilimo, kupitia ukumbatiaji mifumo ya kisasa na teknolojia; mashine, mitambo na vifaa.

Jaya Guru na John George (kushoto), ambao ni waasisi wa kampuni ya Rower, India, wakionyesha mashine aina ya Micron wakati wa Maonyesho ya Kimataifa ya Agritech Africa KICC Nairobi. PICHA | SAMMY WAWERU

Vijana hao, ni magwiji na hodari katika utengenezaji wa mashine za upanzi wa mboga na viungo vya mapishi, za wakulima wa mashamba madogo na yale ya kadri.

Katika maonyesho hayo ya Makala ya saba walifumbua macho waliomiminika, kuhusu mashine aina ya Micron na Hop-5.

Micron ni mashine ndogo, inayopanda mbegu kwa kusukumwa sawa na Hop-5 ambayo ni kubwa kiasi.

Huku Kenya mbinu ya upanzi inayojulikana ikiwa ile ya mkulima kuandaa mashine au mitaro, kisha kupanda mbegu na kufunika, George aliambia Akilimali kwamba mashine hizo zinatekeleza shughuli zote hizo.

“Zinaanda mitaro, kupanda na kufunika,” akasema.

Alisema, baada ya shamba kuandaliwa, mbegu huwekwa kwenye masanduku ya mashine kisha mkulima anaisukuma.

“Nafasi kati ya mbegu, mkulima ndiye anafanya vipimo kupitia mtambo wa gearbox,” George akaelezea.

Fatalaiza au mbolea, mkulima anasambaza mwenyewe shambani kabla kuanza upanzi.

Kulingana na wabunifu hao wanaomiliki kampuni ya Rower, nchini India, mashine inasukumwa na mtu mmoja au wawili.

“Inachukua kati ya saa nne hadi tano kukamilisha ekari moja,” Jaya akafafanua, akihoji inapunguza gharama ya leba kwa karibu asilimia 40.

Mashine hizo aidha ni bora katika upanzi wa kabichi, spinachi, nyanya, giligilani – dhania, pilipili hoho (zile kali), bitiruti, karoti, kati ya mboga na viungo vingine vya mapishi.

Walidokeza kwamba tayari wamepata wafanyabiashara watakaokuwa wakiuza vifaa hivyo nchini, Micron ikigharimu Sh35,000 na Hop-5 Sh110,000.

 

  • Tags

You can share this post!

DKT FLO: Kiharusi cha joto ni maradhi gani?

West Ham United wamvizia Jesse Lingard kutoka Manchester...

T L