Mashine zapokonya wachunaji majanichai kazi

Mashine zapokonya wachunaji majanichai kazi

TOM MATOKE na BARNABAS BII

MAELFU wa wafanyakazi katika sekta ya majanichai wapo hatarini kupoteza kazi zao, baada ya kampuni nyingi kuanza kutumia mashine kuchuma mimea hiyo ili kupunguza gharama ya ulipaji mishahara.

Hii inatokea wakati ambapo bei ya majanichai inaendelea kushuka katika soko la kimataifa kutokana na mataifa mengi kuwasilisha majani yenye ubora wa hali ya juu.

Hali inaendelea kuwa mbaya huku tayari zaidi ya wachumaji 50,000 wa zao hilo wakiachishwa kazi na kukosa njia ya kukimu familia zao.

Muungano wa Kitaifa wa Wakulima na Wafanyakazi katika sekta ya Majanichai (KPAWU) nao umekashifu kampuni tano za majanichai katika eneo la Bonde la Ufa ambazo zimeanza kutumia mashine na kuwafungia nje wachumaji.

Aidha kampuni hizo pia zimewafuta kazi maelfu ya wafanyakazi ili kupunguza gharama ya kuwalipa mishahara.

Naibu Mwenyekiti wa KPAWU Eliakim Ochieng’ jana alidai kuwa usimamizi wa kampuni mbalimbali unalenga kuwatimua wafanyakazi wote na kukumbatia uchumaji wa majanichai kwa kutumia mashine kwa asilimia 100 na tayari zinatumia mashine hizo kwa asilimia 70.Kati ya kampuni ambazo afisa huyo alizitaja ni EPK, Williamson, Sotik, Finlay, Unileaver, Kipkebe.

Kampuni hizo zinapatikana katika kaunti za Kericho, Nandi, Bomet na Nyamira na tangu mwaka jana, zimekuwa zikiwatimua wafanyakazi kwa mwenendo wa kusikitisha.

“Familia nyingi za waliokuwa wachumaji wa majanichai sasa zinaumia kwa sababu kampuni sasa zinatumia mashine kisha kuwafuta wengi kazini,” akasema Bw Ochieng’.

Kutokana na uchumi mbovu na kushuka kwa bei ya majanichai, kampuni nyingi zimekuwa zikilipa Sh28 pekee kwa kilo, malipo ambayo yametajwa kuwa ya chini mno kwa wafanyakazi ambao hujituma licha ya kuwa hatarini kufutwa.

Wakulima nao wanalilia serikali kuwekeza pesa katika sekta ya kilimo cha majanichai ili kukwamua ndipo waepuke hasara kubwa ambayo wamekuwa wakipata.

Kama njia ya kuzuia kampuni kutumia mashine na kuwafungia nje wafanyakazi, Bunge la Kaunti ya Nandi mnamo mwaka jana lilipitisha na kuweka ada za ziada kwa kampuni hizo.

Kwa mujibu wa Mwakilishi wa wadi ya Kapchorwa John Kebenei na mwenzake wa Kabwareng Jackson Swadi, hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa kampuni hizo zinakoma kuwaachishwa kazi wachuma majanichai.

“Kando na hatari ya kiafya, mashine hizo huchangia kupunguza ubora wa majanichai na kuinyima Kenya mapato mengi kwenye soko la kimataifa,” akasema Bw Swadi.

Hata hivyo, Afisa Mkuu wa Muungano wa Wakuzaji wa Majanichai Apollo Kiarii alikanusha madai ya KPAWU kuwa wengi wamepoteza ajira zao kutokana na kuanzishwa kwa matumizi ya mashine hizo.

“Hakuna mfanyakazi ambaye ametimuliwa na kampuni yoyote. Kampuni hazijakuwa zikiwapa kazi wafanyakazi wengine baada ya baadhi kujiuzulu au kufa na badala yake zimekuwa zikitumia mashine kufidia upungufu huo,” akasema.

You can share this post!

‘Wasanii Wazoefu’ mboni ya sanaa chuoni Gretsa, Thika

Spark FC yacharaza Real Stars katika mojawapo ya matokeo...