Habari Mseto

Mashirika kutoa mafunzo kuhusu hedhi kwa wavulana

October 16th, 2020 2 min read

Na DIANA MUTHEU

MASHIRIKA ya kibinafsi katika Kaunti za Mombasa na Kilifi yamependekeza watoto wa kiume wahusishwe katika mafunzo kuhusu hedhi ili kupunguza unyanyapaa katika jamii.

Akisema na Taifa Leo katika mkutano wa kuzungumzia jinsi mashirika hayo yataweza kuunda na kutekeleza sera za usimamizi wa maswala ya hedhi, meneja wa miradi na maswala ya uzazi katika shirika la Dream Achievers Youth Organisation, Bw Gaetano Muganda alisema kuwa swala la afya na hedhi ni la jamii nzima.

“Pakubwa, jamii inakosea kwa kudhania kuwa maswala kuhusu hedhi yanafaa kuelekezewa wanawake pekee. Ni vizuri kujumuisha wanaume na wavulana ili waweze kulielewa swala nzima na pia wawe miongoni mwa watu wanaoleta suluhu kwa changamoto zinazowakumba wasichana na wanawake wanaokosa vifaa muhimu vya kudumisha usafi wakati wa hedhi,” akasema Bw Muganda huku akiongeza kuwa mashirika zaidi ya 10 yaliokuwa katika mkutano huo yatafanya kazi kwa pamoja kuhakikisha kuwa wamefikia malengo yao.

Afisa huyo alitoa maoni kuwa wanaume wakihusihwa na pia kuhamasishwa kuhusu maswala ya hedhi, wataweza kuwa mstari wa mbele kuleta mabadiliko na hata kusaidia katika kupunguza mimba za mapema.

Baadhi ya sababu ambazo zimekuwa zikitajwa na mashirika mbalimbali kama chanzo cha mimba hizo ni ukosefu wa vifaa muhimu vya kutumiwa wakati wa hedhi, ambapo baadhi ya wasichana hujitosa katika ngono ili wapate fedha za kununua bidhaa hizo.

“Wasichana nao wataweza kujivunia swala la hedhi bila ya woga kuwa kutakuweko na aina yeyote ya unyanyapaa,” akasema.

Mshirikishi wa miradi katika shirika la Y-Act ambalo ni tawi katika Shirika la Amref, Bi Joyce Mbuthia alisema kuwa wanaume wengi ndio tegemeo katika familia zao, na hivyo wakihusishwa katika mazungumzo kuhusu hedhi, wataweza kuwasaidia watoto wao wa kike na wake zao pia.

“Nao wavulana shuleni hawatawacheka wasichana ambao huanza kupata hedhi bila kutarajia, bali wataelewa kuwa ni jambo la kawaida msichana au mwanamke kupata hedhi. Pia, watajua la kufanya iwapo dada zao watajikuta katika hali hio bila kutarajia,” akasema Bi Mbuthia.

TAFSIRI NA FAUSTINE NGILA