Habari

Mashirika, viongozi waanza kutoa chakula cha msaada

April 5th, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

SERIKALI za Kaunti, viongozi wa makanisa na mashirika mbalimbali wameanza kutoa vyakula kwa familia zisizojiweza wakati nchi inaendelea kupambana na janga la virusi vya corona.

Serikali ya kaunti ya Mombasa imekusanya Sh13.5 milioni katika mradi utakaohakikisha zaidi ya familia 20,000 zimepata chakula cha msaada iwapo serikali itatangaza marufuku ya kutotoka nyumbani.

Mradi huu ulioanzishwa na Gavana wa Mombasa, Hassan Joho, unatarajia kukusanya zaidi ya Sh700 milioni ambazo zitasaidia kila familia kupata vyakula.

Akiongea Jumamosi wakati wa kuwashukuru wafadhili, wakiwemo wafanyibiashara katika kaunti hiyo, Bw Joho aliwarai watu wengi kujitokeza ili kusaidia, akisisitiza kuwa shughuli hiyo itafanywa kwa uwazi bila mapendeleo yoyote.

“Huu ni wakati wetu kutoa na kusaidiana. Iwapo hali hii itazidi, itabidi tulazimishe watu kukaa nyumbani. Hivyo basi lazima tutafute njia ya kuwasaidia,” Bw Joho alisema.

Kaunti hiyo pia ilisema itahitaji angalau Sh3,380 kulisha familia ya watu watano kila wiki.

Wakazi wanatarajia kupokea kilo 10 za mchele na unga wa ugali. Kilo saba za ndengu, mbili za sukari, lita tatu za mafuta ya kupika na pakiti mbili za sodo.

Visima 30 pia vinatarajiwa kuchimbwa kwa kila wadi ya kaunti hio.

Wakazi pia watapewa dawa za maumivu kwa kila familia baada ya mfanyibiashara mmoja kutoa dawa milioni moja almaarufu Paracetamol.

Kwingineko, katika barua iliyoandikwa Aprili 3 kwa makasisi wa dayosisi ya Mombasa, Askofu Martin Kivuva alisema tayari wameunda kamati ya kushugulikia dharura zinazoletwa na maradhi ya COVID-19, na itakusanya vyakula na fedha.

Pia, itapokea msaada kutoka kwa wasamaria wema, itasambaza bidhaa kwa watu wasiojiweza na kufanya kazi kwa ukaribu na mashirika mengine kuhakikisha wanahamasisha umma kuhusu virusi hivyo.

Katika kijiji cha Kiandutu mjini Thika mnamo Jumamosi, maskini na walemavu wapatao 200 walipokea msaada wa unga na mikate.

Spika wa bunge la kaunti ya Kiambu Bw Stephen Ndichu shughuli ya kusambaza msaada hiyo.

Aliyemwakilisha spika kwenye shughuli hiyo, Bw Francis Kilango, alisema walemavu wengi na maskini katika kijiji hicho wamepitia masaibu mengi huku wengi wao wakikosa chakula cha kila siku.

Alisema wengi wao hawana maji ya kunawa, sabuni, huku wakiwa katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya virusi.

Askofu Kilango alisema kijiji cha Kiandutu ambacho kina idadi ya wakazi zaidi ya 20,000 kinahitaji msaada wa dharura kwa kuwa bado wakazi hao hawazingatii hali ya usafi kutokana na hali ya maisha kuwa ngumu.

Naye mbunge wa Kimilili, Didimus Barasa alinunua magunia 200 ya mahindi yatakayogawanywa kwa familia maskini iwapo marufuku ya kutoka nje itawekwa.

Na katika eneo bunge la Kesses, kaunti ya Uasin Gishu, Mbunge wa sehemu hiyo Swarup Mishra (pichani) alinunua shehena kubwa ya chakula ambacho kitasambazwa kwa wazee katika kaunti hiyo.

Tayari Gavana wa sehemu hiyo Jackson Mandago amepiga marufuku wazee kuingia mijini.

Ripoti za DIANA MUTHEU, SIAGO CECE, LAWRENCE ONGARO na BRIAN OJAMAA