Mashirika yamlaumu DPP kwa kuondoa kesi dhidi ya polisi

Mashirika yamlaumu DPP kwa kuondoa kesi dhidi ya polisi

Na BENSON MATHEKA

Mashirika 18 ya kutetea haki za binamu yamemlaumu Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kwa kuondoa mashtaka dhidi ya maafisa 15 wa polisi walioshtakiwa kwa kudhulumu familia moja kaunti ya Busia mwaka jana.

Mashirika hayo yalisikitika kuwa licha ya Shirika la kuchunguza Utendakazi wa polisi (IPOA) kupendekeza maafisa hao washtakiwe, DPP aliondoa mashtaka dhidi yao na kufifisha matumaini ya familia hiyo kupata haki.

Baada ya kufanya uchunguzi, IPOA ilipendekeza kuwa maafisa hao washtakiwe kwa kuvamia boma la Bw Benard Orenga eneo la Nambale, Busia mnamo Machi 30 2020, wakarusha gesi ya kutoa machozi na kumpiga na kumjeruhi pamoja na mkewe na watoto wake.

IPOA ilipendekeza kuwa waliohusika wafunguliwe mashtaka ya kupiga, kujeruhi na kuharibu mali maksudi.

Kundi la mashirika yanayopigania mageuzi katika kikosi cha polisi la Police Reforms Working Group Kenya (PRWG-K) linasema kwamba maafisa hao walitarajiwa kujibu mashtaka Jumatatu lakini DPP alifahamisha mahakama kwamba ameondoa kesi dhidi yao.

“Kama PRWG-K, tunaamini kwamba maafisa wa polisi wanaotumia vibaya mamlaka yao ni lazima wachunguzwe na kushtakiwa. Kenya itakaribia utawala wa sheria wakati wote wanaoshukiwa kuikiuka, wakiwemo maafisa wa polisi watashtakiwa na kupatiwa nafasi ya kujitetea katika mahakama ya kikatiba,” mashirika hayo yalisema kwenye taarifa.

Yalimtaka DPP kubadilisha nia ya kuondoa mashtaka dhidi ya maafisa hao ili waathiriwa waweze kupata haki.

Miongoni mwa mashirika yaliyotia saini taarifa hiyo ni Transparency International, Amnesty International, Independent Medico Unit (IMLU), Kenya Human Right Commission, Katiba Institute, Haki Afrika, Shied for Justice, Usalama Kenya na Internation Justice Mission.

You can share this post!

Sonko atupwa ndani siku tatu

Joho na Kingi waongoza mipango ya kuhama ODM