Mashirika yataka adhabu kali kwa wauaji wa wazee

Mashirika yataka adhabu kali kwa wauaji wa wazee

NA ALEX KALAMA

MASHIRIKA ya kutetea haki za kibinadamu katika Kaunti ya Kilifi yameshinikiza idara ya Usalama pamoja na taasisi nyingine husika za serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria wahusika wa mauaji ya wazee kwa tuhuma za uchawi.

Wakizungumza mjini Malindi katika maadhimisho ya siku ya amani uliwenguni, wanaharakati hao wakiongozwa na mwenyekiti wa kamati ya usalama na amani, kaunti hiyo, Bi Merab Shibuyanga, wamezitaka haki za wazee kulindwa.

“Tunataka kuona hatua ikichukuliwa na watu wakifungwa kwa sababu ya mauaji,” akasema Bi Shibuyanga.

Mwanaharakati Merab Shibuyanga akiwa katika kampeni za kukomesha mauaji ya wazee Malindi. PICHA | ALEX KALAMA

Kwa miaka mingi, kumekuwa na malalamishi miongoni mwa jamii mbalimbali za Pwani kuhusu mauaji ya wazee wanaodaiwa kuwa wachawi.

Licha ya idara za usalama kuhusisha mauaji hayo na mizozo ya ardhi za kifamilia, baadhi ya maafisa wa usalama hulalamika wale wanaotegemewa kuwa mashahidi huwa hawajitolei kusaidia katika uchunguzi na kutoa ushahidi mahakamani.

Hali hii hulaumiwa kama sababu ya kuachiliwa huru kwa washukiwa huku wazee wengi wakihama makwao na kutafuta hifadhi maeneo mengine salama.

Bw Bimkala Kitibwa, aliyenusurika kifo alipovamiwa nyumbani kwake mapema mwaka huu 2022 kutokana na tuhuma hizo za uchawi alisema bado huhisi hayuko salama hata katika makao ya wazee ambapo anaishi.

Mzee Bimkala Kitibwa, mmoja wa manusura ambaye amehifadhiwa katika kituo cha Moi ndiye huyo aliyevaa shati la rangi ya kijani. PICHA | ALEX KALAMA

Ameiomba serikali na wadau mbalimbali kuziwekea ua sehemu ambazo zimetengwa kuwalinda wazee wanapokuwa hatarini makwao ili kuwakinga na uvamizi.

“Machoni mwangu bado ninaona wale walionitafuta ili kuniua kule kwangu wanaweza kuingia hata hapa wakati wowote. Maanake nyumba hazina milango na pia hakuna ua,” alisema Bw Kitibwa.

Kwa upande wake msaidizi wa naibu kamishna katika eneobunge la Malindi, Bi Angela Wanyama, amewataka wakazi wa eneo hilo kutumia njia mbadala za kisheria kusuluhisha mizozo ya kifamilia badala ya kuwaua wazee.

Msaidizi wa naibu kamishna Malindi Bi Angela Wanyama akihutubia wanahabari. PICHA | ALEX KALAMA

Aliwaomba wakazi wa kaunti hiyo kuondoa dhana potofu za kuwahusisha wazee na ushirikina.

“Hasa hapa Malindi tumezingatia eneo moja ambapo tunasema uzee si uchawi, kwa sababu walikuwa wanauliwa sehemu hizi za Malindi kwa kisingizio kuwa ni wachawi. Serikali tunahimiza wanainchi wa Malindi, tuko na njia nyingi sana ambazo tunaeza kutumia ili kutatua mizozo isiwe vita,” alisema Bi Wanyama.

Mbali na Kaunti ya Kilifi, sehemu nyingine ambapo wazee wamekuwa wakipitia hali ngumu kwa kudaiwa kuwa wachawi ni Kwale na Kisii.

Baadhi ya wazee wakiwa katika kituo cha kuhifadhi wazee katika kijiji cha Moi kilichoko Malindi, Kaunti ya Kilifi. PICHA | ALEX KALAMA
  • Tags

You can share this post!

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Dunia ya leo yahitaji dua kwa wingi...

DOMO: Wakati mwingine tuache ujinga

T L