Habari MsetoSiasa

Mashirika yataka Wakenya wahusishwe kubadili Katiba

March 17th, 2019 2 min read

NA CECIL ODONGO

VIONGOZI wa Mashirika ya Kijamii (NCSC) Jumapili waliwataka Wakenya kushirikishwa vilivyo kwenye mjadala unaoendelea wa marekebisho ya Katiba na kuwakemea viongozi wa kisiasa wanaopigania maslahi yao kuhusu marekebisho hayo.

Hata hivyo, walisisitiza kwamba Katiba lazima ifanyiwe marekebisho ili kuleta suluhisho la masuala tata kama chaguzi na ugavi sawa wa mapato ya kitaifa.

Rais wa mashirika hayo Morris Odhiambo alisema wadau wote wanafaa kufahamu kuwa marekebisho ya Katiba yanawahusu Wakenya na haki zao wala si maslahi ya viongozi wachache ambao sifa zao za uongozi tayari zimetiwa doa na kufeli mtihani wa maadili.

“Mjadala unaoendelea wa kurekebisha Katiba ni muhimu ingawa inasikitisha kwamba viongozi wanapigania maslahi yao bila kuzingatia mambo yanayonufaisha mwananchi. Mwaka wa 2010 Wakenya waliachia viongozi wao jukumu la kusoma Katiba ila mara hii lazima wahusishwe kikamilifu ili maslahi yao yazingatiwe,”

“Kila Mkenya ana haki ya kutoa wazo lake kuhusu marekebisho hayo ila kwa mtazamo wetu mjadala huu haufai kulenga ujenzi wa himaya ya viongozi wachache wenye nia ya kutetea maslahi yao,’’ akasema Bw Odhiambo.

Akizungumza na wanahabari jana jijini Nairobi, Bw Odhiambo alisema uongozi wa NCSC utatumia tajriba na uzoefu kutoka kwa kampeni za awali za kura ya maamuzi kama Yes- Yes Katiba (2007-2008), Katiba Sasa! (2008-2009) na Katiba Initiative (2010-2016) kuhakikisha unatimiza wajibu wake wa kuwahusisha Wakenya katika mchakato mzima wa kurekebisha Katiba na kura ya maamuzi inayotarajiwa kuambatana na shughuli hiyo.

Mashirika hayo jana yalizindua nguzo nane za kutathmini mapendekezo yanayopigiwa upatu kujumuishwa kwenye marekebisho hayo.

Baadhi ya nguzo hizo ni uwazi katika vita dhidi ya ufisadi, usawa wa kijinsia na ulemavu, usawa wa utoaji huduma katika ngazi mbili za serikali zilizopo, kuheshimu haki ya raia ya kujieleza na Wakenya kuhusishwa katika masuala yaliyo na umuhimu kitaifa.

Nyingine ni uimarishaji wa demokrasia na uwazi katika matokeo ya uchaguzi, kupunguzwa kwa gharama za kuendesha serikali za kaunti na kitaifa na hakikisho kuwa Wakenya wanatangamana na kuishi kwa amani.