Habari Mseto

Mashujaa wa Mau Mau kutunukiwa mashamba

December 13th, 2018 1 min read

Na CHARLES WANYORO

SERIKALI ya kaunti ya Embu imeanza kuwakagua wazee wanaodai kuwa walipigana katika vita vya Mau Mau, ili kubaini watakaonufaika na shamba la ukubwa wa ekari 44,000, eneo la Mwea.

Gavana Martin Wambora amesema kuwa serikali yake inapitia orodha ya wazee ambayo ilikusanya kutoka kaunti nzima, na kuwa kila mpiganaji atapokea ekari tano za shamba.

Akizungumza wakati wa sherehe za Jamhuri katika uwanja wa Runyenjes, gavana huyo alisema wametenga ekari 100 kwa mashujaa hao, akisema kuwa wanataka kuhakikisha watakaofaidika ni wale tu wapiganaji halisi wa Mau Mau.

Alisema kuwa serikali yake iko makini kuhakikisha kuwa wapiganaji waliosalia wanapewa mashamba na kuwajengea manyumbani kabla yao kufa.