Michezo

Masikitiko ya Oliech kuhusu viwango vya soka nchini Kenya

September 6th, 2019 4 min read

Na MWANGI MUIRURI

SOGORA Dennis Oguta Oliech kwa sasa akiwa katika masaibu ya kitaalumu na klabu ya Gor Mahia almaarufu K’Ogalo ‘Sirkal’ anasema kuwa Kenya iko mbali sana na kuafikia viwango vya kimataifa katika mchezo wa soka.

Akiwa na tajiriba ya kuchezea ligi kubwa nje ya nchi na rekodi nzuri ya kuwa kidedea katika kutikisa nyavu akiwajibikia Harambee Stars ambapo kwa sasa ana magoli 34, Oliech anasema tamanio lake na ni kuona wachezaji wa soka Kenya wakifaulu kwenda Ulaya, Bara Hindi na kwingineko.

“Tuna uwezo huo ila tu kinachoturudisha nyuma ni ukosefu wa sera, ufisadi na ubutu wa usimamizi,” anasema Oliech.

Akisisitizia Taifa Leo kuwa bado yuko na makali ya kuwika ugani kwa sasa akiwa na umri wa miaka 35, anasema kuwa miundombinu ya mchezo huu wa soka hapa nchini ni duni na pale kidogo kuna afueni, siasa zisizofaa huvuruga mambo.

“Mchezaji wa soka Kenya huchukuliwa tu kama kifaa cha kutumika kikihitajika. Wakati mchezaji anahitajika kuwakilisha taifa, ndipo unapata kila aina ya sarakasi za kutambua soka hapa nchini. Unapata ndio wanasiasa wameanza kuahidi pesa na wengine wakiahidi kila aina ya minofu hewa kwa Harambee Stars,” anasema.

Anasema kuwa hakuna mikakati ya kuwadumishia wachezaji chipukizi viwango vyao vya kipawa kinapotambulika na huishia katika hali kwamba wanasoka nchini hawana tegemeo katika kujenga taaluma nchini bali ni lazima waondoke hadi nchi za ng’ambo.

“Ukienda taifa la Afrika Kusini, utapata kwamba ligi yao ya taifa ya soka ina ushindani mkali na unaweza ukajenga hata timu tano kutoka kwa wachezaji wa ligi ya nyumbani. Hapa Kenya, ni vigumu hata kujenga wachezaji 11,” anasema.

Oliech ambaye kwa sasa ametemwa nje na usimamizi wa Gor katika mzozo wa kandarasi anasema kuwa atastaafu akiwa na umri wa miaka 37 au 38 na ambapo amedokeza kuwa anasaka kandarasi na klabu mbadala, kipaumbele kikiwa ni kutua Wazito FC, Mathare United FC au AFC Leopards.

Aidha, amesisitiza kuwa ikiwa klabu ya Gor haitamlipa marupurupu yake yote ya kandarasi ya miaka minne basi atahakikisha amepata ilani ya mahakama ya kushinikiza alipwe, uongozi wa Gor nao ukishikilia kuwa alitemwa nje kufuatia utovu wa nidhamu na ambapo sheria hata za shirikisho la kandanda duniani FIFA huzima mwanya wa kulipwa fidia katika msingi wa kukatiziwa mkataba katika hali ya utovu wa nidhamu.

Oliech anateta kuwa “huu ndio udhalimu wa soka hapa nchini ambapo hakuna hata ushauriano, watu huamka na kufanya yao bila kuhusisha wadau na hatimaye hali inaishia kuwa ya vurugu.”

Anasema kuwa ameumia mkono na wasimamizi wa Gor walifaa kushauriana na hata daktari wa timu ili kubaini ni kwa ini hakuwa akihudhuria mazoezi.

Mizozo ya kila mara

Oliech anasema kuwa mizozo hiyo ndiyo huishia hata timu ya taifa kuwa katika mizozo ya kila mara na makocha, klabu za soka kuishiwa na makali ya usimamizi thabiti huku wengi ndani ya mchezo huu wakiwa wanasaka njia na namna za kujipa shibe.

“Ukiuliza Mkenya wa kawaida nembo ya timu ya Harambee Stars ni gani, hajui. Hatujui hata sare rasmi ya Harambee Stars ni gani. Masilahi ya wachezaji Kenya hayana wa kuyajali na ndio tuna aibu ya vipawa murwa ambavyo vingewika kimataifa ila leo hii viko katika magereza ya Kenya kama wafungwa, wengine wakiwa katika madanguro na wakijihusisha na ulevi na mihadarati,” anasikitika.

Oliech anasema kuwa Baraka kuu ya Kenya ni kuwa “wananchi wanapenda soka na huunga mkono timu na wachezaji kikamilifu lakini kwa shirikisho na serikali, kukijidhihirisha mgongano na ubutu wa hali ya juu.”

Akisema analenga kuwania wadhifa katika shirikisho la kandanda nchini ili achangie mabadiliko ya kina ya kufaa sekta ya soka nchini, Oliech anasema kuwa Harambee Stars kwa sasa itabakia ikimenyania ubabe wa Jumuiya ya Afrika Mashariki lakini katika viwango vya Afrika na ulimwengu, ibaki ikiyumba.

Anasema kuwa kwa sasa kungekuwa na kamati ya kushughulikia urekebishaji wa udhaifu uliojitokeza katika mechi za Harambee stars katika jukwaa la michuano ya taifa bora Africa (Afcon 2019) na pia kuthibiti yale mazuri yalijidhihirisha lakini “tumekaa kimya tukingoja hali ya karata ya pata potea kuhusu Afcon 2021.”

Anasema kuwa wachezaji wa Kenya hawana mpango thabiti wa malipo, kandarasi na masilahi kama bima ya afya kushughulikia matibabu endapo wataumia ugani.

Ni katika hali hii ambapo Gavana wa Murang’a, Mwangi wa Iria ametoa maoni yake kuwa serikali kuu ihamishie timu ya kitaifa ya soka, Harambee Stars hadi usimamizi wa serikali za Kaunti kwa kuwa magavana wako na uwezo wa kuandaa timu hiyo kuibuka bora zaidi Afrika kupitia mikakati ya ufadhili.

Wa Iria anashikilia kuwa ni aibu kubwa kuwa Harambee Stars ina muundo butu uliojaliwa kile anataja ni ukabila na mapendeleo katika uteuzi wa timu na ndiyo sababu kuu ya kuadhibiwa mara kwa mara katika mechi za hadhi.

“Sisi kama Kaunti tunaweza tukachanga pesa za kufadhili timu ya Harambee Stars. Tupewe nafasi ya kusaka vipaji vya soka, tuwape bima na mishahara, tulipe kocha wa kiwango cha kimataifa na tuwapambe wanasoka hao na jezi rasmi ya Kenya. Tulio nao katika usimamizi wa soka hapa nchini sio wa kutegemewa katu,” akasema.

Wa Iria alisema kuwa timu ya soka ya taifa inafaa kuonyesha usawa wa usajili wa wachezaji ndio Wakenya wajipe nafasi ya kushabikia utaifa ndani ya timu hiyo.

“Wewe enda usake orodha ya wachezaji wa Harambee Stars na uniambie kama hiyo ni timu ya Kitaifa. Uniambie kama ni timu ya kimaeneo au ni ile ya wakenya. Tuko na vipaji katika jamii nyingi hapa nchini lakini kuna ile kasumba kuwa gozi liko na wenyewe,” akasema.

Oliech anapendekeza kuwa wadau wakome unafiki na watoe vifaa na ufadhili kwa utunzaji vipawa na vifaa ugani na Kenya katika kipindi kidogo cha mwaka mmoja itakuwa na sifa za kiulimwengu.