Masit adai kushurutishwa afuate nyayo za wenzake na ajiuzulu

Masit adai kushurutishwa afuate nyayo za wenzake na ajiuzulu

NA CHARLES WASONGA

MMOJA wa Makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) waasi Irene Masit amedai kushurutishwa na mtu asiyejulikana kwamba ajiuzulu.

Kupitia wakili wake, Donald Kipkorir, kamishna huyo, ambaye ndiye amesimama kidete baada ya wenzake watatu kujiondoa, aliambia jopo linalomchungumza kwamba alipokea simu kutoka kwa mwanamke, akimtaka ajiuzulu Ijumaa.

“Mteja wangu alipokea simu kutoka kwa mtu asiyemjua, japo sauti yake ilikuwa ya kike, akimtisha kwamba ajiuzulu. Hii ina maana kuwa suala hili linasukumwa na watu ambao wanayo nia fiche,” akasema Bw Kipkorir, Ijumaa Desemba 9, 2022 wakati wa kikao cha kwanza cha jopo lilibuniwa kumchunguza.

Jopo hilo linaloongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa Aggrey Muchelule liliteuliwa na Rais William Ruto kuchunguza uhalali wa ombi la kutaka Masit, na wenzake,  watimuliwe afisini.

Hata hivyo, baada ya kuundwa kwa jopo hilo, makamishna watatu Justus Nyang’aya, Juliana Cherera na Francis Wanderi, walijiuzulu mmoja baada ya mwingine.

Kwenye kikao hicho cha kwanza cha jopo hilo , Bi Masit pia  aliomba asichunguzwe kwa misingi kuwa wenzake watatu walikuwa wamejiondoa.

Wakili wake alisema hatua ya jopo hilo kuendelea kumchunguza baada ya wenzake watatu kujiuzulu hakutakuwa ya haki kwa sababu wangetumia stakabadhi sawa katika kujitetea.

“Kwa sababu makamishna watatu wamejiuzulu, kuendelea na shughuli hii hakutamtendea haki mteja wangu haki kwa sababu stakabadhi za kujitetea na ushahidi zimeandaliwa pamoja,” Kipkorir akasema.

Hata hivyo, Bw Muchelule alitupilia mbali ombi hilo na kushikilia kuwa kila moja ya makamishna hao, hata wale waliojiuzulu wakachunguzwa kivyao.

“Kila mmoja aliateuliwa kivyake, ilikuwa ni uteuzi wa kibinafsi na kiapo cha kila mmoja kwa mujibu wa katiba. Maombi ya kuondolewa kwa makamishna pia yaliwasilishwa kuhusu kila mmoja wao,” Bw Muchelule akasema kwenye uamuzi wake.

Kamishna Nyang’aya ndiye alikuwa wa kwanza kujiuzulu Ijumaa wiki jana, akafuatwa na Bi Cherera mnamo Jumatatu ilhali Bw Wanderi alijiondoa Alhamisi.

Baada ya mkutano wa maandalizi wa jopo hilo uliofanyika Ijumaa, Desemba 9,2022, liliahirishwa vikao vyake hadi Desemba 20.

Jopo hilo lilichukua hatua hiyo ili kutoa nafasi kwa kesi iliyowasilishwa na Masit kusitisha kuchunguzwa kwake, isitikizwe na kuamuliwa.

Hata hivyo, wakili Kipkorir alielezea matumaini kuwa mteja wake ataepuka madhila yanayomkabili.

“Haijali ni lini, Kamishna Irene Masit hatapatikana na makossa. Haki haina makataa au muda wa kutolewa kwake huwa haumaliziki,” Bw Kipkorir akasema kupitia twitter.

Makamishna hao wanne walipinga matokeo ya urais iliyotangazwa na mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati mnamo Agosti 15, 2022 katika ukumbi wa Bomas of Kenya, Nairobi.

Walidai kutohusishwa katika hatua za mwisho za ujumuisha wa kura za urais, shughuli ambayo walidai iliendeshwa “pasina kuzingatia uwazi.”

Mapema mwezi huu, Bunge la Kitaifa liliidhinisha ripoti ya Kamati yake ya Sheria (JLAC) ilipendekeza kutimuliwa kwa wanne hao.

Kamati hiyo iliandaa ripoti hiyo baada ya kuchunguza uhalali wa maombi maane yaliyowasilishwa bunge yakidai Bi Cherera na wenzake hawafai kuendeleza kushikilia afisi zao kwa misingi ya hatua hiyo ya kupinga matokeo ya uchaguzi.

Chama cha Repulican Liberty Party, Kasisi Denis Nthumbi, Bw Geoffrey Lang’at na Steve Jerry Owuor walidai kitendo cha wanne kuashiria uvunjaji wa Katiba, matumizi mabaya ya mamlaka yao, na kutokuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Aidha, walidai kuwa makamishna hao nusra watumbukize taifa hili katika machafuko kupitia kitendo chao cha kukataa matokeo hayo ya urais.

Kwa hivyo, kulingana na wao, Bi Cherera alipaswa kupigwa kalamu.

You can share this post!

Rais Ruto awasilisha ombi la marekebisho ya Katiba...

Visa vya wizi wa mita za maji vyakithiri Malindi

T L