Habari Mseto

Maskauti wa Mlima Kenya wahimiza wakulima wapande miti aina ya mianzi 'bamboo'

July 3rd, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

MASKAUTI wa kutoka eneo la Mlima Kenya wamejitolea kuhamasisha wakulima umuhimu wa kupanda miti aina ya mianzi; yaani bamboo, ili kuzuia athari hasi za mafuriko ya kila mara.

Mnamo Aprili 2018, wakazi wapatao 1,000 wa Murang’a waliachwa bila makao baada ya maporomoko kutokea maeneo tofauti.

Ni kutokana na masaibu ya aina hiyo ndipo wanaskauti hao mnamo Jumanne, waliamua kujitokeza wazi ili kuhamasisha wakulima umuhimu wa upanzi wa miti za bamboo.

Kamishna wa maskauti Kaunti ya Kiambu, Bw Francis Chege Nyoike, alisema ni muhimu kwa wakulima kupokea mawaidha kuhusu upanzi wa miti aina ya bamboo.

Washiriki katika shughuli ya upanzi wa miti eneo la Mlima Kenya. Picha/ Lawrence Ongaro

“Ili kuzuia mmomonyoko wa udongo wakati wa mvua ya masika, litakuwa jambo la busara kupanda miti ya bamboo kwa wingi ili kuzuia maporomoko ya udongo katika makazi ya watu, ” alisema Bw Nyoike.

Alisema miti  hiyo ni muhimu sana katika kuzuia kupotea kwa udongo wakati wa mvua.

Aliyasema hayo mnamo Jumanne katika uwanja wa Pavilion katika Chuo cha Mount Kenya mjini Thika wakati wa upanzi wa miti.

“Sisi kama maskauti tumejitolea vilivyo kuona ya kwamba wakulima wanapata hamasisho ili kuzuia janga la maporomoko ya ardhi katika maeneo husika katika nyanda za juu,” alisema Bw Nyoike.

Mazao

Alisema pia watafanya hamasisho kuhusu upanzi wa mazao yanayostahimili ukame.

Alitaja mazao hayo kama mihogo na viazi.

Afisa mkuu wa mazingira katika Chuo cha Mount Kenya, Bw Benjamin Afumbwa, alisema watazidi kushirikiana na maskauti na mashirika mengine ili kuhifadhi mazingira na kuhamasisha wananchi.

“Chuo cha Mount Kenya kinatumia kiwango kukubwa cha fedha ili kuona ya kwamba kimehifadhi mazingira kila sehemu katika eneo pana la Mlima Kenya na maeneo mengine,” alisema Bw Afumbwa.

Mmamo siku hiyo miti 500 ilipandwa huku watu wengi wakihudhuria hafla hiyo iliyojumuisha wanafunzi wa shule.