Habari Mseto

Maskwota kulipa kanisa Sh500, 000 wasifurushwe

March 31st, 2024 2 min read

NA PHILIP MUYANGA

MASKWOTA wanaoishi ndani ya ardhi ya ekari 40 inayomilikiwa na kanisa Katoliki mjini Voi, watalazimika kulipa kanisa hilo Sh500, 000 kama fidia kwa kuingia humo bila idhini.

Hii ni baada ya rufaa yao dhidi ya uamuzi wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi kutupiliwa mbali.

Mahakama ya Rufaa ilikubali uamuzi wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi, ikisema kuwa rufaa ya maskwota hao haikuwa na msingi wowote na haikuwa imepata jambo lolote kukosoa mahakama hiyo kwa kukubali kesi ya kanisa dhidi yao (maskwota).

Mahakama ya Mazingira na Ardhi ilikuwa imeamua kuwa wadhamini waliosajiliwa wa Jimbo Kuu la kanisa Katoliki Mombasa, ambao ndio wamiliki wa ardhi hiyo, wanafaa kufidiwa kwa kunyimwa nafasi ya kutumia ardhi yake kwa zaidi ya miaka kumi.

Pia, mahakama hiyo ilitoa agizo la kudumu la kuzuia maskwota kubakia au kuendelea kuwa katika ardhi hiyo.

Majaji wa Mahakama ya Rufaa Mumbi Ngugi, George Odunga na Kibaya Laibuta, walisema kuwa maskwota hao waliishi sehemu wazi katika ardhi hiyo vile ilivyodaiwa.

“Kama watu waliokuwa wamepewa leseni na manispaa ya Voi na ikichukuliwa kuwa kanisa lilichukua hatua na kudai haki yake ya umiliki ndani ya mwaka mmoja wa umiliki wa ardhi hiyo kuhamishwa kwake, wakata rufaa walishindwa kuthibitisha kuwa wamiliki kupitia kuishi huko zaidi ya miaka 12 bila kusumbuliwa,” Mahakama ya Rufaa ilisema.

Iliongeza kusema kuwa kipande cha ardhi kilichokuwa kikizozaniwa na wakata rufaa, hakikumaanisha kuwa walikuwa wamiliki kwa njia ya kuishi kwa zaidi ya miaka 12 ilivyodaiwa.

Katika rufaa yao, maskwota hao walisema kuwa Mahakama ya Mazingira na Ardhi ilikuwa imekosea kusema kuwa ingawa ardhi hiyo ilikuwa haina mtu wakati ikipeanwa mwaka wa 1995, haikuwa inamaanisha hakuna wanaoimiliki.

Waliongeza kusema kuwa Mahakama ya Mazingira na Ardhi ilikuwa imekosea kupata kuwa hakukuwa na ushahidi wa kuwa walikuwa wametoa kanisa hilo katika umiliki.

Kulingana na maskwota hao, mahakama hiyo, ilikosea iliposema kuwa walikuwa wamekubali mamlaka ya iliyokuwa manispaa ya Voi.

Kanisa kupitia mawakili wake lilikuwa limepinga rufaa hiyo ya maskwota.

Mahakama ya Ardhi na Mazingira ilikuwa imeagiza maskwota hao watoke kwa kipande hicho cha ardhi kwa muda wa siku 30 baada ya agizo kutolewa.

“Kukosa kufuata maagizo, kanisa litakuwa huru kupata agizo la kuwatoa maskwota hao kwa nguvu kutoka kwa ardhi hiyo likiwasilisha maombi mahakamani,”alisema Jaji Yano.

Katika uamuzi wake, mahakama hiyo, ilisema kuwa kulingana na mikutano baina ya pande zote mbili pamoja na maafisa wa serikali, kanisa lilikuwa tayari kuwapatia ekari saba lakini maskwota walikataa wakidai ulaghai na kwamba eneo hilo lilikuwa majimaji lakini hawakutoa stakabadhi zozote kuthibitisha madai hayo.