Dimba

Masogora wa Arsenal wapunga unyunyu kujisahaulisha msimu mwingine mgumu

June 1st, 2024 2 min read

NA CHRIS ADUNGO

BAADA ya msimu mwingine mgumu wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kumalizika wakiwa nambari mbili jedwalini, nyota wa Arsenal walipata nafasi ya kuvinjari na kupiga sherehe.

Ingawa kikosi cha Mikel Arteta kilifurahia rekodi ya kushinda mechi nyingi zaidi katika kampeni za msimu mmoja ligini, ufanisi huo wa kihistoria haukutosha kumaliza ukame wa mataji Emirates.

Baadhi ya nyota wa Arsenal walianza likizo huku wengine wakihiari kupumzika kwa wiki chache kabla ya kujiunga rasmi na timu zao za taifa kwa michuano ya Euro itakayoanza Juni 14 nchini Ujerumani.

Kunao walioelekea visiwani Maldives kusini mwa bara Asia na familia zao huku wengine wakienda likizo katika nchi zao.

Kai Havertz na Martin Odegaard waliondoka pamoja Uingereza na kufufuliza hadi ufuo wa Ibiza nchini Uhispania wakiandamana na wapenzi wao – Helene Spilling na Sophia Weber mtawalia.

Odegaard alipakia kwenye Instagram picha aliyopigwa akiwa karibu na Havertz huku akijilaza kwenye kitanda cha jua kabla ya picha nyingine kumuonyesha akisisimuana kimapenzi na Helene akiwa kifua wazi.

Havertz naye alirusha mitandaoni video kadhaa akimpiga busu demu wake aliyeketi naye ndani ya mashua na kuandika: “Kuchaji tena!”
Gabriel Jesus kwa upande wake alisherehekea bathidei ya bintiye, Helena, ambaye sasa ametimu miaka miwili.

Aliandaa karamu kubwa iliyohitaji kila ambaye alihudhuria kuvalia mavazi ya rangi nyekundu na kubeba puto nyekundu.

Declan Rice aliamua kuunda hela zaidi kwa kutia saini dili ya kuwa balozi mvumishaji wa huduma na bidhaa za kampuni ya Men’s Health UK. Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na kiungo mvamizi Bukayo Saka.

Kipa David Raya alionekana na mpenzi wake Tatiana Trouboul wakihudhuria harusi ya rafiki yao mmoja nchini Uhispania kabla ya kuelekea Maldives.

Thomas Partey alipiga hatua zaidi katika safari yake ya kimapenzi kwa kumvisha kidosho Janine Jackson pete ya uchumba. Alifanya hivyo katika eneo fulani la ufukweni ambako mashabiki wengi mitandaoni walikisia ni Mauritius.

Thomas Partey na mchumba wake Janine Jackson. Picha|Maktaba

Aaron Ramsdale aliamua kusalia nyumbani kwa mapumziko kabla ya kuungana na kikosi cha Uingereza kwa maandalizi ya mechi za Euro.

Naye Gabriel Martinelli aliamua kutumia likizo yake kujaribu masuala ya uvuvi anapojiandaa kuongoza Brazil katika mechi za Copa America.

Oleksandr Zinchenko alipata nafasi ya kurudi nyumbani kwao Ukraine na kuzuru jiji la Kyiv lililoathiriwa pakubwa na mashambulio ya Urusi.

Alipigwa picha akiwa na rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, nje ya ikulu.

Jorginho na mchumba wake Catherine Harding kwa upande wao walinaswa na kamera wakiwa kwenye harusi ya rafiki yao huko Barcelona, Uhispania. Kiungo huyo mkabaji alikuwa amevalia suti nyeupe pepepe.