Habari

Masoko Ruiru kufungwa kwa siku 21 kuzuia kuenea kwa Covid-19

March 26th, 2020 2 min read

Na SAMMY WAWERU

MASOKO yote eneobunge la Ruiru, Kiambu, yametakiwa kufungwa kwa muda wa siku 21 ili kuzuia na kudhibiti maenezi zaidi ya Covid-19.

Kwenye barua rasmi iliyotumwa na msimamizi wa kaunti ndogo ya Ruiru, Stephen Kiiru kwa wakuu wa masoko yote eneo hilo, imeamriwa yafungwe kufikia leo Alhamisi, Machi 26, 2020.

Mkuu huyo wa kaunti ndogo ya Ruiru ametaja soko la Ruiru Mjini, masoko ya Githurai ndiyo Jubilee na Migingo pamoja na wanaochuuza kandokando mwa barabara, kufungwa mara moja.

“Kufuatia hali iliyopo, hasa kigezo cha umbali baina ili kulinda maisha ya binadamu na kwa mujibu wa sheria zinazodhibiti chakula, dawa na chembechembe za kemikali kifungu Cha 254 (LK), masoko yaliyotajwa yafungwe kufikia Alhamisi Machi 26, 2020 kwa muda wa siku 21,” inaeleza notisi ya barua hiyo iliyotazamwa na ‘Taifa Leo’.

Hii ina maana kuwa masoko hayo yana hadi mwisho wa siku ya Alhamisi kuendesha shughuli za biashara.

Tangu kisa cha kwanza cha Covid – 19 kuripotiwa nchini mapema mwezi huu wa Machi, wafanyabiashara wamekadiria hasara katika kile wanataja kama kiwango cha mauzo kushuka. “Janga la Corona limesababisha biashara kudorora,” akasema Simon Kagombe, mfanyabiashara katika soko la Jubilee.

Licha ya amri ya masoko Ruiru kufungwa kutolewa, baadhi ya wafanyabiashara wanashangaa watakavyoweza kukithi mahitaji yao ya kimsingi, wakidai wanategemea shughuli za biashara kujiendeleza. “Tungeruhusiwa tuendelee kutafutia familia zetu ila tuzingatie usafi na umbali baina yetu na wateja,” akapendekeza mchuuzi mmoja wa vitunguu, akiongeza kusema kwamba amri iliyotolewa itakwamisha uchumi.

Hata hivyo, kuna wanaounga mkono agizo hilo, Mzee Njenga ambaye ni mmoja wa wasimamizi wa soko la Jubilee akifafanua kuwa kila mmoja hana budi ila kufuata utaratibu na maagizo yaliyotolewa ili kama taifa tushirikiane kudhibiti maenezi ya virusi hivyo hatari.

Thika

Masoko ya Thika yalifungwa mnamo Jumanne.

Gavana wa Kiambu James Nyoro amesisitiza lazima masoko yote kaunti hiyo yafungwe, akisema “sharti utaratibu, kanuni na sheria za serikali ziheshimiwe ili tufanikishe kudhibiti ueneaji zaidi wa Covid-19”.

Waziri wa Afya Mutahi Kagwe amesema visa vya maambukizi zaidi yanayoshuhudiwa vinajiri kwa kile ametaja kama baadhi ya Wakenya “kukosa maadili” na kupuuza utaratibu uliotolewa kuzuia maenezi ya Covid-19.

Kufikia sasa Kenya imethibitisha visa 28 vya maambukizi ya virusi hivyo vya corona, Rais Kenyatta Jumatano akitangaza kuwa mgonjwa mmoja amepona.