Masomo yatatizika Lamu shule zikiwahifadhi waliokwepa mashambulio vijijini

Masomo yatatizika Lamu shule zikiwahifadhi waliokwepa mashambulio vijijini

NA KALUME KAZUNGU

SHUGHULI za masomo zimeathirika pakubwa kwenye maeneo ya Lamu ambayo yamekuwa yakishuhudia ghasia na mauaji yanayotekelezwa na wahalifu wanaoshukiwa kuwa ni wapiganaji wa Al-Shabaab huku mamia ya wanafunzi wakisalia nyumbani ilhali wengine wakiishi kwenye kambi za wakimbizi.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo juma hili ulibaini kuwa karibu wanafunzi 1,500 wamesalia nyumbani na wazazi wao baada ya shule zaidi ya tano, zote zikiwa za msingi kufungwa kutokana na utovu wa usalama Lamu.

Baadhi ya wanafunzi pia hawajakanyaga madarasani hasa baada ya shule zao kugeuzwa kuwa kambi za muda za wakimbizi waliokwepa ukatili wa wapiganaji wa Al-Shabaab.

Mashambulio yaliyoanza kushuhudiwa tangu Januari 2, 2022 tayari yameacha watu 15, ikiwemo maafisa wanne wa polisi wa kitengo cha GSU wakifariki ilhali nyumba zaidi ya kumi zikiteketezwa moto.

Akizungumza na Taifa Leo, Afisa wa Elimu wa Lamu Magharibi, John Nzinga, alithibitisha kuwa shule za msingi za Juhudi, Salama, Kibaoni Shalom Academy na Holy Angels zilizoko tarafa ya Mpeketoni zimesalia kufungwa katika kipindi cha juma moja lililopita kufuatia utovu wa usalama.

Mahudhurio ya wanafunzi kwenye shule jirani za msingi, ikiwemo Mikinduni, Majembeni, Muhamarani na Bahati Njema pia yamekuwa duni wiki yote kutokana na kwamba baadhi ya wanafunzi waliandamana na wazazi wao kuhamia kwenye kambi za wakimbizi wa ghasia zinazoendelea.

Bw Nzinga alisema ofisi yake tayari imefanya majadiliano na kamati ya usalama Lamu ili kuona kwamba shule hizo zinafunguliwa kufikia juma lijalo.

“Karibu shule tatu zimefungwa kabisa ilhali nyingine zikigeuzwa kuwa kambi za muda za wakimbizi. Mahudhurio pia hayajakuwa ya kuridhisha kwenye shule zetu za mashambani kutokana na zogo la utovu wa usalama.Mipango ipo ili kufungua shule zote ambazo kwa sasa zimekosa kuhudumu kufikia juma lijalo,” akasema Bw Nzinga.

Baadhi ya wamiliki wa shule,hasa zile zilizogeuzwa kambi za wakimbizi waliitaka serikali kusaidia taasisi hizo kwa miundomsingi ili kutosheleza mahitaji ya wakimbizi wanaoishi hapo.

Mmiliki wa Shule ya Msingi ya Kibinafsi ya Shalom Academy mjini Kibaoni, Amon Chengo, alisema zaidi ya familia 250 za wakimbizi zimepiga kambi shuleni humo katika kipindi cha juma moja lililopita na kwamba hakuna shughuli zozote za kimasomo ambazozinaendelea kufikia sasa.

“Tulisitisha masomo tangu wiki iliyopita. Familia za wakimbizi zimepiga kambi shuleni hapa. Wanafunzi wangu wote 150 wamesalia nyumbani.Miundomsingi hapa, ikiwemo madarasa na vyoo havitoshi kukimu idadi kubwa ya wakimbizi. Serikali na wahisani watusaidie kuimarisha hali hii. Pia wasaidie wakimbizi wapate mahali mbadala na salama pa kuishi ili kupisha masomo kuendelea shuleni kwangu angalau kufikia wiki ijayo,” akasema Bw Chengo.

Kwa upande wake, Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia alishikilia kuwa usalama umeimarishwa kote Lamu na kwamba ni vyema waliotoroka vijiji vyao kurudi mara moja.

Kulingana na Bw Macharia, serikali bado inaendeleza makabiliano na wahalifu, hivyo kuwataka wananchi kuondoa hofu.

“Watu waache kuhama vijijini na kukaa kambini. Serikali imejitolea kulinda wananchi wake popote walipo, ikiwemo kule vijiji mashambani. Ni vyema watu warudi kwenye mashamba yao,” akasema Bw Macharia.

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali ifanye juhudi kuzima mauaji ya watu

KIMANI NJUGUNA: Wakenya wajifunze na kuchagua viongozi...

T L