Masonko waelezea sababu kuunga Raila kidole

Masonko waelezea sababu kuunga Raila kidole

Na WANDERI KAMAU

MABWANYENYE wa eneo la Mlima Kenya jana walimwidhinisha rasmi kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, kama mwaniaji watakayemuunga mkono kwenye uchaguzi wa urais mwaka ujao.

Chini ya Wakfu wa Mlima Kenya (MKF), mabwanyenye hao waliorodhesha sababu ambazo zimewafanya kumkumbatia Bw Odinga.Bw Odinga anatarajiwa kuzindua rasmi azma yake ya kuwania urais kesho katika Uwanja wa Michezo wa Kasarani, huku Rais Uhuru Kenyatta akitarajiwa kuhudhuria.

Kwenye kikao kilichofanyika katika mkahawa mmoja jijini Nairobi, mabwanyenye hao walimtaja Bw Odinga kama kiongozi wanayemwamini ataendeleza na kulinda maslahi ya eneo hilo, ikiwa atachaguliwa kuwa mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta.

Miongoni mwa masuala waliyopendekeza ayashughulikie ni uboreshaji sekta ya kilimo kwa kuimarisha bei za mazao kama kahawa na majani chai, kuongeza kiwango cha fedha kinachotengewa eneo hilo kulingana na wingi wa wenyeji, kukabiliana na ulevi, kuondoa mivutano iliyopo baina ya wazee na vijana, kuwatafutia makao mbadala watu waliofurushwa makwao kutokana na ghasia (IDPs), kubuni mazingira mwafaka kwa wenyeji kufanyia biashara kati ya mengine.

“Tunamtaka kiongozi atakayetuhakikishia atatimiza na kuendeleza maslahi yetu. Baada ya utathmini wa kina kuhusu viongozi wote waliojitokeza kuwania urais, tulimpata Bw Odinga kuwa chaguo bora zaidi. Ndiye kiongozi tunayehisi atatutimizia na kulinda matakwa yetu,” akasema Wazri wa Kilimo, Peter Munya, ambaye alisoma maamuzi hayo kwa niaba ya mabwanyenye hao.

Chini ya mwavuli wa Wakfu wa Mlima Kenya (MKF), walimsifia Bw Odinga kuwa kiongozi “shujaa aliyejitolea pakubwa kutetea ukombozi wa nchi.”“Hatutaki kuwa chini ya viongozi wenye historia mbaya kama vile uporaji wa mali ya umma, unyakuzi wa ardhi na uchochezi wa ghasia.

Tunataka kuongozwa na watu wapenda amani na wanaoheshimu jamii zote nchini,” akasema Bw Munya, huku akishangiliwa na watu walioshiriki.Kwenye kauli iliyoonekana kumlenga Naibu Rais William Ruto, mabwanyenye hao pia walisema hawataki uongozi wa “mtu atakayedai kulimiliki eneo hilo.

”“Sisi ndio viongozi tuliopo. Hatutaki kuwa chini ya mtu atakayedai kuwa kiongozi wa eneo hilo bila kutuomba ushauri au kutushirikisha kikamilifu,” wakasema waziri. Mwishoni mwa Oktoba, mabwanyenye hao walifanya vikao tofauti na Bw Odinga na vinara wa OKA, wakisema walifanya hilo “kuwapiga msasa” kuhusu kiongozi bora ambaye wangemuunga mkono.

Kando na mabwanyenye hao, Bw Odinga amepata uungwaji mkono wa magavana wa eneo hilo, wakiwemo Francis Kimemia (Nyandarua), Kiraitu Murungi (Meru), Muthomi Njuki (Tharaka-Nithi), Lee Kinyanjui (Nakuru) na Nderitu Mureithi (Laikipia).Bw Odinga amekuwa akizuru kaunti hizo chini ya mwaliko wa magavana hao.

You can share this post!

IEBC yaonya Raila, Ruto kuhusu kampeni

TAHARIRI: IEBC ihakikishe wanasiasa wanaoshiriki harambee...

T L