Michezo

Masoud Juma ajiondoa Stars ikijiandaa dhidi ya Msumbiji

October 3rd, 2019 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

FOWADI Masoud Juma amejiondoa katika kikosi cha Harambee Stars kinachotazamiwa kuanza maandalizi kwa ajili ya mchuano wa kirafiki dhidi ya Mambas ya Msumbuji baadaye mwezi huu wa Oktoba.

Nyota wa kikosi cha JS Kabylie nchini Algeria, alikuwa sehemu ya wavamizi ambao kocha Francis Kimanzi alipania kuongoza safu ya mbele ya Stars katika mechi mbili zijazo za kirafiki dhidi ya Msumbuji na Libya.

Washambuliaji wengine waliotazamiwa kushirikiana na Juma ni Michael Olunga wa Kashiwa Reysol nchini Japan na Jesse Were wa Zesco United nchini Zambia.

Kwa mujibu Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), kujiondoa kwa Masoud kunachochewa na jeraha la goti alilolipata wakati akiwawajibikia waajiri wake wikendi iliyopita.

“Juma hatakuwa sehemu ya kikosi cha Stars kitakachopimana nguvu na Msumbuji katika mchuano ujao wa kirafiki. Klabu yake ya Kabylie imethibitisha kwamba anauguza jeraha la goti litakalomweka nje kwa muda sasa. Nafasi yake itatwaliwa sasa na Enosh Ochieng wa Ulinzi Stars,” ikasema sehemu ya taarifa.