Habari Mseto

Maspika wa kaunti waahidi kutoa msimamo huru kuhusu 'Punguza Mizigo

July 31st, 2019 2 min read

Na SAM KIPLAGAT na WANDERI KAMAU

MAHAKAMA Kuu imesimamisha mabunge 47 kujadili na kuidhinisha mswada wa Punguza Mizigo ulioasisiwa na chama cha Thirdway Alliance Kenya.

Jaji James Makau pia amekisimamisha chama hicho akisema hakifai kuwasilisha mswada huo kwa Spika wa Bunge la Kitaifa, hadi kesi iliyowasilishwa mahakamani isikilizwe na kuamuliwa.

Jaji alisema maagizo hayo yatadumishwa kwa kipindi cha wiki mbili hadi wengine waliotajwa katika kesi hiyo watakapoweka wazi kwa mahakama mawasilisho yao.

 

Chamahicho kupitia kwa Elias Mutuma kilipinga maagizo, kikisema kilipewa muda mchache tu, siku moja, kuwasilisha mahakamani.

Wakili aliambia mahakama kwamba angalau siku tatu zingefaa.

Na wakati huo huo, mnamo Jumanne, maspika wa mabunge ya kaunti walisema watachukua msimamo wao kuhusu Punguza mizigo bila shinikizo zozote.

Baraza la Maspika wa Kaunti (CAF) Jumanne lilisema kuwa halitashawishiwa na yeyote kutoa msimamo wao kuhusu Mswada wa Punguza Mizigo, unaoendeshwa na chama cha Thirdway Alliance.

Mwenyekiti wa baraza hilo Bw Ndegwa Wahome, alisema kwamba, wanashauriana na mawakili wao wa kikatiba, ili kuhakikisha msimamo watakaotangaza utazingatia matakwa ya wananchi.

Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi, baraza hilo lilisema kuwa, lengo lake ni kuhakikisha kuwa msimamo litakaotoa utalingana na maoni ya wananchi wengi.

“Hatutashawishiwa na yeyote kutoa msimamo wetu. Ikumbukwe kuwa mabunge ya kaunti ndiyo yatakuwa na usemi mkuu kwenye maamuzi ya mswada huo. Tunashauriana na wadau mbalimbali kabla ya kutangaza rasmi msimamo wetu,” akasema Bw Wahome.

Tayari, vyama vya ODM na Wiper vimetoa misimamo yao rasmi kuhusu mswada huo.

Wiki iliyopita, ODM, ilikosoa mswada huo, ikisema haujatoa utaratibu wa ushirikishi katika Serikali Kuu na njia itakayotumiwa kukabili deni la kitaifa ambalo linazidi kuongezeka.

Umma

Kwa upande wake, Wiper ilikosoa chama cha Thirdway Alliance, ikisema hakikuushirikisha umma katika uandaaji wa mswada huo.

Hata hivyo, walisema kwamba wanaunga mkono pendekezo la kuongezwa kwa mgao wa fedha za kaunti kutoka kwa serikali ya kitaifa, kwani ni baadhi ya mambo ambayo wamekuwa wakipigania.

“Ingawa hatujatoa msimamo rasmi, utathmini wetu wa mwanzo mwanzo kuhusu mswada huu ni kwamba, unaashiria hatua nzuri kwa masuala ambayo tumekuwa tukiyapigania kama Wakenya. Tutayashirikisha mabunge yote 47 ili kuutathmini kwa undani,” akasema Bw Wahome.

Wanachama wengine waliokuwepo katika kikao hicho ni Naibu Mweyekiti, Bi Florence Mwangangi, Katibu Mkuu Kipkurui Chepkwony,  Naibu Katibu Mkuu Bi Rebah Wabwire, Katibu Mshirikishi Bi Florence Oile, Naibu Katibu Mshirikishi Bw Adamson Lanyasunya na Bw Ahmed Ibrahim, ambaye ni mwekahazina.

Viongozi hao pia waliomba usuluhishaji wa haraka wa mzozo uliopo kati ya Bunge la Kitaifa na Seneti kuhusu upitishaji wa Mswada wa Ugavi Fedha kwa Serikali za Kaunti.