Michezo

Mastaa wa Shujaa waingia Simbas kuitafutia tiketi Kombe la Dunia

October 23rd, 2018 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

WACHEZAJI wote kutoka timu ya Shujaa walioitwa katika timu ya Simbas wamepata namba kupeperusha bendera ya Kenya katika mchujo wa kufuzu kushiriki Kombe la Dunia mwaka 2019 nchini Japan.

Collins Injera, Nelson Oyoo, Samuel Oliech na Andrew Amonde, ambao walijumuishwa katika Simbas mwezi Septemba, wameridhisha kocha kutoka New Zealand Ian Snook kiasi cha kumpa imani kwamba wakishirikiana na wengine, watafanyia Kenya kazi nzuri katika mchujo huo dhidi ya Canada, Hong Kong na Ujerumani.

Wanne hawa wanaungana na nahodha wa zamani wa Simbas Wilson K’opondo, ambaye aling’aa katika timu ya Shujaa mwaka 2009. K’opondo anarejea baada ya mwaka mmoja. Oliech aling’aa sana akichezea Simbas mwaka 2015 kabla ya kunyakuliwa na Shujaa.

Snook ametaja kikosi cha wachezaji 30 kitakachovaana na Canada mnamo Novemba 11, Hong Kong hapo Novemba 17 na Ujerumani mnamo Novemba 23. Mshindi wa mchujo huu wa mataifa manne ataingia Kombe la Dunia litakalofanyika nchini Japan mwaka 2019. Atamenyana na New Zealand, Afrika Kusini, Italia na Namibia katika Kundi B.

Sura nyingine mpya katika kikosi cha Simbas ni William Reeve, ambaye alimvutia Snook wakati wa mashindano ya kitaifa ya raga ya wachezaji saba kila upande yaliyofanyika kutoka Julai 21 hadi Septemba 16 mwaka 2018.

Mchezaji huyu kutoka klabu ya Kenya Harlequin pia ameng’aa katika mashindano ya Impala Floodlit. Nyota wa Shujaa na Harlequin, William Ambaka pia yuko kikosini. Ambaka alicheza mechi mbili za mwisho za Simbas kwenye Kombe la Afrika mwezi Agosti ambapo Kenya ililima Tunisia 67-0 jijini Nairobi kabla ya kulemewa na Namibia 53-28 katika fainali jijini Windhoek.

Simbas itaondoka nchini Oktoba 31 kuelekea nchini Romania kupitia nchini Ufaransa kwa mechi ya kirafiki itakayosakatwa jijini Bucherest mnamo Novemba 3. Itarejea nchini Ufaransa mnamo Novemba 6 kukabiliana na Canada, Hong Kong na Ujerumani mjini Marseille.

Kikosi cha Simbas:

Washambuliaji

Patrick Ouko (Homeboyz), Moses Amusala (KCB), Joseph Odero (Kabras Sugar), Hillary Mwanjilwa (Kabras Sugar), Ephraim Oduor (Kabras Sugar), Colman Were (Kabras Sugar), Philip Ikambili (Homeboyz), Oliver Mang’eni (KCB), Wilson K’opondo (Kenya Harlequins), Malcolm Onsando (Kenya Harlequins), Simon Muniafu (Impala Saracens), Andrew Omonde (KCB), George Nyambua (Kabras Sugar), Dalmus Chituyi (Homeboyz), Elkeans Musonye (Strathmore Leos), Joshua Chisanga (Homeboyz), Davis Chenge (KCB) na Martin Owilah (KCB);

Walinzi

Samson Onsomu (Impala Saracens), Mohammed Omollo (Homeboyz), Samuel Oliech (Impala Saracens), Darwin Mukidza (KCB), Leo Seje Owade (Impala Saracens), Peter Kilonzo (KCB), Collins Injera (Mwamba), Nelson Oyoo (Nakuru), Felix Ayange (Kabras Sugar), William Ambaka (Kenya Harlequins), Tony Onyango (Homeboyz) na William Reeve (Kenya Harlequins)

Benchi la kiufundi: Ian Snook (Kocha Mkuu), Murray Roulston (Kocha), Wangila Simiyu (Meneja wa Timu), Charles Ngovi (Naibu Kocha), Dominique Habimana (Naibu Kocha), James Ondiege (Daktari wa timu), Christopher Makachia (Daktari) na Edwin Boit (mtathmini wa timu).