Michezo

Mastaaa wa Kariobangi kujiunga na Yanga

April 20th, 2020 2 min read

NA CHRIS ADUNGO

KARIOBANGI Sharks wamekiri kwamba hawatawazuia nyota wao wawili Sven Yidah na Harrison Mwendwa kujiunga na Yanga SC nchini Tanzania mwishoni mwa msimu huu.

Yidah na Mwendwa wamekuwa katika rada ya Yanga tangu mwaka jana na kwa sasa wako pua na mdomo kujiunga na miamba hao wa Ligi Kuu ya Tanzania.

Robert Maoga ambaye ni mwenyekiti wa Sharks amesisitiza kuwa watakuwa radhi kuwaachilia wachezaji wao hao kutafuta fursa mpya za kujikuza kitaaluma japo wangali na mikataba nao. Yidah angali na mwaka mmoja katika kandarasi yake na Sharks huku Mwendwa akisalia na miaka miwili zaidi.

“Yanga walianza kuwamezea mate wachezaji wetu hawa mwaka jana tulipokuwa nchini Tanzania kwa minajili ya kivumbi cha Super Cup kilichoandaliwa jijini Dar es Salaam. Hata hivyo, bado hatujapokea ofa yao rasmi. Tutazitathmini ofa hizo pindi watakapoziwasilisha,” akasema Maoga.

Hadi kivumbi cha Ligi Kuu ya Kenya (KPL) ilipositishwa kwa muda mwanzoni mwa mwezi jana kutokana na hofu ya maambukizi zaidi ya corona, Mwendwa alikuwa akishiriki mazoezi na vijana wa umri usiozidi miaka 20 kambini mwa Sharks.

Kwa mujibu wa Maoga, maamuzi hayo yaliafikiwa baada ya makali ya fowadi huyo mvamizi kushuka.

“Benchi ya kiufundi ilibaini kwamba kiwango chake cha ubora kilikuwa kimeshuka baada ya kutatizwa na majeraha. Hivyo, hatua ya kumjumuisha katika kikosi cha chipukizi ilipania kumwamshia upya hamasa ya kupigania nafasi yake katika kikosi cha kwanza,” akaongeza Maoga.

Kwa upande wake, meneja wa timu ya Yanga SC, Dis Masten amefichua kwamba wamepiga hatua kubwa katika kuwashawishi Yidah na Mwendwa kujiunga nao na kufikia sasa dalili zote zinaashiria kwamba juhudi zao zitazaa matunda kufikia Juni 2020.

“Hawa ni wachezaji wa haiba kubwa ambao ujio wao utatuwezesha kuyafikia mengi ya maazimio yetu katika misimu kadhaa ijayo,” akasema Masten ambaye pia alichangia pakubwa kufanikisha uhamisho wa kipa Farouk Shikalo kutoka Bandari FC hadi Yanga mnamo Juni 2019.

Yidah aliyekosa mechi nne zilizopita za Sharks, ni miongoni mwa wachezaji ambao wamehudumu kambini mwa kikosi hicho kwa kipindi kirefu zaidi na amevalia jezi za waajiri wake hao mara 97 katika mashindano yote tangu aagane na Ligi Ndogo.