Habari

Maswali 10 ya 'Tangatanga'

September 27th, 2020 2 min read

Na WANDERI KAMAU

MRENGO wa ‘Tangatanga’ Jumamosi uliitaka serikali kujibu maswali 10 kuhusu mpango wa kuwasajili upya Wakenya kupitia mfumo wa ‘Huduma Namba’, ukidai uwepo wa njama za wizi wa kura na uporaji wa fedha za umma.

Serikali ilieleza kuhusu mpango wa kuwasajili Wakenya ambao hawakusajiliwa kwenye awamu ya kwanza ya shughuli hiyo kufikia Desemba mwaka huu.

Lakini Jumamosi, karibu wabunge 10 wa mrengo huo, ambao humuunga mkono Naibu Rais William Ruto, waliitaka Serikali kueleza kuhusu dharura ya kurejelea usajili huo, wakidai unaendeshwa kwa njia ya siri.

Wabunge hao walijumuisha Kimani Ichung’wah (Kikuyu), Ndindi Nyoro (Kiharu), John Kiarie (Dagoretti Kusini), Nixon Korir (Lang’ata) miongoni mwa wengine.

Kwenye kikao na wanahabari katika hoteli moja jijini Nairobi, wabunge hao walishangaa sababu ya kutoa zabuni ghali ya mpango huo “kwa njia fiche”.

“Mbona mchakato wa utoaji tenda kuhusu mchakato unaendeshwa kisiri badala ya njia ya wazi kama ilivyo kwenye Katiba? Mbona idara husika hazijashirikishwa?” wakadai viongozi hao, katika taarifa iliyosomwa na Bw Kiarie.

Vilevile, waliitaka serikali kueleza sababu ambapo kampuni moja ya kigeni imelipwa Sh7 bilioni kuendesha mpango huo. Walidai serikali imeiteua kampuni ya Muhlbauer High Tech International (au Muhlbauer ID Services GmbH) kuendesha mchakato huo.

Walidai kuwa watu wawili, waliowataja kama Matthias Karl Kohler na H Karashani wamekuwa wakifanya vikao na baadhi ya wafanyakazi wa Idara ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS).

Walisema wawili hao wamekuwa wakikaa katika hoteli moja ya kifahari jijini Nairobi kwa wiki moja iliyopita, huku wakizuru makao makuu ya NIS kwa muda huo wote.

Waliwataja wawili hao kuwa mamluki huku wakitaka ufafanuzi kuhusu aliyelipa gharama za kuwasafirisha nchini, ulinzi wanaopewa na aliyegharimia malipo yao kwenye hoteli waliokaa walipowasili nchini.

“Ili kuonyesha umuhimu kuhusu mpango huu, wawili hao walipewa ulinzi mkali kutoka kwa vikosi maalum vya usalama kwa siku tano walizokaa nchini,” akadai Bw Kiarie.

Dai lingine walilotaka majibu ni kuhusu kujumuishwa kwa afisa waliyemtaja kama Dkt Mativo kutoka NIS kama Mkurugenzi Mkuu wa Mpango wa Usajili wa Huduma Namba.

Aidha, waliitaka Serikali kueleza yaliyojadiliwa kwenye mikutano waliyodai ilifanyika mnamo Septemba 11 na 14 mtawalia.

Wabunge hao pia walishangaa kuhusu hatua ya mradi huo kuondolewa kutoka Wizara ya Usalama wa Ndani hadi chini ya usimamizi wa NIS.

“Ikizingatiwa wizara hiyo imesema kampuni zote zitakazohusika kwenye mpango huo ni za hapa nchini, mbona isitueleze asili ya kampuni ya Muhlbauer High Tech International?” akaeleza.

Walisema kuwa kwa mchakato huo kuendelea, lazima serikali itoe maelezo yote kuhusu Wakenya waliosajiliwa kwenye awamu ya kwanza ya mchakato huo.

Hata hivyo, chama cha ODM kiliyapuuza madai hayo, kikiyataja kama yasiyo na msingi, kwani Dkt Ruto alikuwa miongoni mwa maafisa wakuu serikalini waliojitokeza kusajiliwa kwenye awamu ya kwanza mwaka uliopita.

Kupitia Katibu Mkuu Edwin Sifuna, chama hicho kiliyataja madai hayo kama dalili ya kuogopa kushindwa kwenye uchaguzi mkuu wa urais wa 2022.