Habari Mseto

Maswali chungu nzima baada ya kifo cha Papa Dennis

February 9th, 2020 1 min read

Na MARY WANGARI

Wingu la huzuni liligubika tasnia ya muziki kufuatia kifo cha mwimbaji maarufu, Dennis Mwangi, almaarufu Papa Dennis aliyefariki katika hali ya kutatanisha usiku wa kuamkia Jumamosi. 

Mwili wa mwimbaji huyo wa kibao cha injili kilichovuma Nashukuru, ulipatikana kando ya barabara eneo la Ngara Nairobi, mnamo Ijumaa usiku.

Kiini cha kifo chake hakikuweza kubainika mara moja huku baadhi ya ripoti zikiashiria huenda alijitoa roho kwa kujirusha kutoka ghorofa ya saba ya jumba moja mtaani Ngara. Baadhi ya watu walishuku kwamba msanii huyo aliuawa na watu wasiojulikana.

“Sawa na vifo vya wanafunzi wa Kakamega, kisa hiki pia kinaibua maswali mengi. Haidhuru, lala salama Papa Dennis,” aliandika Dan Masoni.

Baadhi ya walioshuhudia walisema kwamba marehemu alikuwa akifanya mazoezi katika studio ya Nairobi Records inayomilikiwa na prodyusa Mash Mjukuu, kabla ya kufululiza nje na kuanguka kutoka ghorofa ya saba na kufariki papo hapo.

“Kuna cha mno zaidi mbali na kujitoa uhai. Hata kama ni kujiua, kuna kitu ndani ya studio kilichosababisha tukio hilo. Hilo si jengo pekee lililo refu ikiwa angetaka kujiua,” Bernad Koech alihoji.

Msanii huyo aliyempoteza mama yake mnamo 2006, amemwacha kaka yake pacha na ndugu wengine wawili.

Mnamo Juni 17, 2018, marehemu alihusika katika ajali mbaya ya barabarani ambapo gari lake liliharibika vibaya na kumwacha akiuguza majeraha hospitalini.

Mwanamuziki huyo aliyefahamika kwa maisha yake ya kifahari- akimiliki gari zuri, mavazi na mapambo ya thamani, alitunukiwa tuzo kadhaa katika taaluma yake ya uimbaji.

Mnamo 2018, alinyakua Tuzo ya Jarida la Muziki Afrika (AFRIMAMA) huku akishinda Tuzo ya Pulse kuhusu Video mnamo 2017 na 2016 na Mwafaka 2015.

Aidha, muziki wake ulitamba kimataifa huku akifanikiwa kushirikiana na wanamuziki wengine mashuhuri kama vile Ray C wa Tanzania na msanii Mr Flavour wa Nigeria.