Maswali chungu nzima baada ya vigogo wa Azimio kususia mkutano wa Azimio uwanjani Kamukunji

Maswali chungu nzima baada ya vigogo wa Azimio kususia mkutano wa Azimio uwanjani Kamukunji

NA CHARLES WASONGA

INGAWA mkutano wa muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya uliofanyika katika uwanja wa kihistoria wa Kamukunji, Nairobi uliibua msisimko mkubwa, baadhi ya vigogo wake waliukwepa.

Ilitarajiwa kuwa kiongozi wa muungano huo Raila Odinga alipangiwa kuachilia “bomu” la kisiasa katika hotuba yake, haswa kuhusu ufichuzi uliodai kuwa ndiye aliyeshinda katika uchaguzi wa urais, 2022.

Bw Odinga amekuwa nchini Amerika kwa wiki moja katika ziara ya kikazi ya wadhifa wake wa Mjumbe wa Umoja wa Afrika (AU) kuhusu Miundomsingi.

Ingawa mkutano wa Kamukunji ulihudhuriwa na vigogo kama kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua, Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni na Eugene Wamalwa, vigogo wengine hawakuwepo.

Wao ni pamoja na; Katibu Mkuu wa Azimio Junet Mohamed, mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi, Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe na Seneta wa Narok Ledama Ole Kina.

Wengine ni: Naibu Kiongozi wa ODM Ali Hassan Joho, mwenyekiti wa kitaifa wa chama hicho John Mbadi, na Mbunge wa zamani wa Gatanga Peter Kenneth.

Mwingine ambaye hakuwepo ni kiongozi wa Narc Charity Ngilu na magavana wote waliochanguliwa kwa tiketi ya vyama tanzu katika Azimio.

Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga anahudhuria mkutano wa mashauriano kuhusu Kamati ya Baraza la Magavana kuhusu Ardhi, Nyumba na Maendeleo unaendelea Mombasa.

Magavana wengine wandani wa karibu wa Bw Odinga ambao hawakuhudhuria mkutano huo ni; Abdulswamad Sheriff Nassir (Mombasa), James Orengo (Siaya), Anyang’ Nyong’o (Kisumu) miongoni mwa wengine.

Ni siku ambapo mkutano huo ulifanyika ambapo wabunge kadha wa Jubilee kutoka Mlima Kenya walimtembelea Rais Ruto katika Ikulu, ishara ya kujitolea kwao kushirikiana kisiasa na mrengo wa Kenya Kwanza.

Wakiongozwa na Mbunge wa Afrika Mashariki (EALA) Kanini Kega na Mbunge Maalum Sabina Chege wabunge hao walisema hawataunga mkono siasa za makabiliano za Bw Odinga.

Wengine waliokutana na Rais Ruto ni; Irene Njoki (Bahati), Zachary Kwenya Thuku ( Kinangop), Shadrach Mwiti (Imenti Kusini), Mark Mwenje (Embakasi Magharibi), Amos Mwago (Starehe), Dan Karitho ( Igembe ya Kati), Stanley Muthama ( Lamu Magharibi) na Seneta wa Lamu Joseph Githuku.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Mageuzi yajayo katika HELB yafanywe kwa umakinifu

Wanaraga wa KCB watolewa jasho wakipiga Strathmore Leos...

T L