Siasa

Maswali Gachagua akikwepa hafla muhimu za kitaifa

May 18th, 2024 1 min read

NA ROSELYNE OBALA

KUKOSEKANA kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua wakati Rais William Ruto alimkaribisha mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni katika ziara ya kiserikali ni mojawapo ya matukio tisa mfululizo ambayo yanaibua maswali kuhusu aliko kiongozi huyo anayeshikilia wadhifa wa pili wa juu nchini.

Kwa kawaida, Wakenya wamezoea kumuona Bw Gachagua karibu na mkubwa wake katika shughuli muhimu.

Mara ya mwisho kuonekana hadharani kwa Bw Gachagua ilikuwa Jumatatu katika Soko la Kagumo, Kaunti ya Kirinyaga—siku moja tu baada ya kufufua mjadala wa ugavi wa mapato kwa kutegemea idadi ya watu- mtu mmoja, kura moja, shilingi moja.

Hakujakuwa na mawasiliano ya umma kuhusu aliko Bw Gachagua ikiwa yuko mapumzikoni au safarini.

Naibu Rais aliibua sintofahamu Ijumaa wiki iliyopita kwa kukosa wakati wa kampeni ya kitaifa ya kupanda miti iliyohusisha Rais na Mawaziri katika maeneo mbalimbali nchini.

Awali, alikuwa amepangwa kupanda miti katika Kaunti ya Bomet, lakini inasemekana alibadilisha dakika za mwisho huku maafisa kutoka ofisi yake wakiwa tayari uwanjani.

Bw Gachagua pia alikosekana katika kikao cha Ikulu cha Jumanne wakati Rais alikutana na wenyeviti na wakurugenzi wa mashirika muhimu ambapo walikubaliana kutekeleza Jopokazi la Chai kushughulikia mizozo miongoni mwa washikadau.

Marekebisho katika sekta ya chai, maziwa na kahawa ni miradi ya naibu rais, baada ya kukabidhiwa jukumu na mkubwa wake.

Baada ya kukosa, Rais alimuagiza Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei, kushughulikia suala hilo.

Bw Koskei alitumia mtandao wa kijamii wa X, ambao zamani ulikuwa ukiitwa Twitter, akiashiria kwamba alichukua jukumu hilo kwa maagizo ya mkubwa wake.