Makala

Maswali kuhusu miili 247 iliyofikishwa City Mortuary wakati wa maandamano

Na COLLINS OMULO August 5th, 2024 2 min read

MAKAFANI ya Nairobi (City Mortuary) ilipokea miili 247 ndani ya mwezi moja wakati ambapo maandamano dhidi ya Mswada wa Fedha 2024 yalikuwa yamefika kilele chake mwezi uliopita.

Kwa mujibu wa Afisa Mku wa Afya ya Umma Nairobi Tom Nyakaba, makafani hiyo hupokea miili 40 kwa wastani kila mwezi. Kupokea miili 247 ambayo ni idadi ya juu sana kunaibua maswali kuhusu takwimu kamili kuhusu waliouawa wakati wa maandamano hayo.

Kwa mujibu takwimu iliyonakiliwa kati ya Juni 25 na Julai 26 iliyotegemea sajili ya polisi, mochari hiyo ina miili 115 ambayo utambulizi wake haujulikani.

Kati ya idadi hiyo, 60 bado ipo kwenye hifadhi hiyo ya maiti na jamaa zao bado hawajajitokeza wala hawafahamu kama wapendwa wao waliaga dunia.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, miili mingine ilikuja ikatambuliwa baada ya jamaa zao kujitokeza.  Idadi ya miili iliyosalia ni sehemu za miili ya wale ambao walipatikana kwenye mkasa wa mauaji ya wengi Kware (17).

Aidha vijusi 13 (foetus) pia ipo katika makafani hayo kulingana na data hiyo iliyotengenezwa na Mwanapatholojia wa serikali Dkt Sylvester Maingi.

Idadi hiyo ya juu ya miili iliyofikishwa katika mochari hiyo ilitokea wakati ambapo Gen Z nao walikuwa wamekaba koo utawala wa Rais William Ruto wakitaka ubanduke mamlakani.

Vijana hao maarufu kama Gen Z walijibwaga barabarani kupinga pendekezo la nyongeza ya ushuru ambalo lilikuwa kwenye Mswada wa Fedha 2024.

Maandamano hayo ambayo yalianza katikati mwa Juni yalisababisha maafa ya watu 60 kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Shirika la Kutetea Hazi Kibanadamu (KNCHR).

Ripoti ya KNCHR ilionyesha kuwa watu wengine 66 walikuwa wametoweka huku waliokamatwa wakiwa 1,376.  KNCHR ilisema maandamano hayo yalifanyika katika kaunti 23 ambapo maafa mengi yaliripotiwa Nairobi ikiwa na vifo 21.

Watu 29 na zaidi kwa mujibu wa KNCHR walikufa katika kaunti nyingine na kuzua masuali zaidi kuhusu miili ambayo ilipelekwa makafani ya Nairobi.

Magatuzi ambayo yaliripoti vifo ni Nakuru (3), Laikipia (2), Narok (1), Kajiado (3), Uasin Gishu (4), Kakamega (2), Kisumu (3), Kisii (1), Mombasa (3), Siaya (1), Kiambu (1), Nandi (1), Embu (1), Homa Bay (1), Nyeri (1) na Bungoma (1).

Katika kilichoibua maswali zaidi, Dkt Maingi alidai kuwa walioaga dunia kutokana na maandamano, walitambuliwa, miili yao ikafanyiwa upasuaji, bili ya mochari ikafutwa na miili ikakabidhiwa jamaa waende waizike.

“Kutokana na maelezo kutoka kwa vituo vya polisi, naamini kuwa miili ambayo bado haijatambuliwa na ileletwa mochari hii, haihusiani na mauti yaliyotokea wakati wa maandamano,” akasema Dkt Maingi.

“Kwa hivyo, taarifa ambazo zimeenea katika vyombo vya habari ni uongo na hakuna ushahidi wa kuzithibitisha,” akaongeza.

Mwanapatholojia huyo alikuwa akizungumzia habari za shirika moja la kupigania haki za kibinadamu kuwa kuna miili mingi katika mochari ya city kando na ile ambayo ilitolewa Kware na ilikuwa na majeraha ya risasi.

“Baadhi ya miili hiyo ina majeraha ya risasi na tunawaomba wale ambao jamaa zao bado hawajapatikana wafike makafani ya city kuangalia miili iliyoko kama ni wao,” akasema Hussein Khalid, wakili na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la VOCAL Afrika.

Kwa wastani mochari hiyo hupokea miili saba kila siku kwa mujibu wa mahojiano yaliyofanyika mnamo Septemba 2021 na Mkuu wa Makafani ya City Dkt David Wanjohi. Afisa huyo alisema kuwa mnamo Agosti mwaka huo walipokea miili 60 ambayo ilikuwa ya chini zaidi ikilinganishwa na hali ya kawaida.

Habari za uwepo wa miili hiyo sasa inaiweka serikali pabaya wakati ambapo Mamlaka Huru ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi (IPOA) imelalamika kuwa polisi hawashirikiani nao wakati ambapo wanachunguza dhuluma na kutumiwa kwa nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji.

  • Imetafsiriwa na Cecil Odongo