Habari Mseto

Maswali yaibuka kuhusu ubomozi wa nyumba Zimmerman

May 6th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

WAMILIKI wa majengo katika mradi wa shamba la chama cha ushirika cha Zimmerman Settlement Scheme, lililoko Nairobi, wamepata afueni baada ya serikali ya kaunti kusimamisha ubomozi wa nyumba.

Shamba hilo linalodaiwa kuwa la maskwota linapakana na Thika Super Highyway ambapo ubomozi wa nyumba, zingine za kifahari na soko, ulianza mwezi uliopita japo ukasitishwa kwa muda.

Ubomoaji ulipaswa kurejelewa, ikidaiwa maafisa wa polisi walikuwa wamekusanyika katika kituo cha polisi cha Kasarani wakipanga mikakati ya kusimamia shughuli hiyo.

Baadhi ya nyumba zilizobomolewa. Picha/ Sammy Waweru

Ni kufuatia hilo ambapo wamiliki na wabunge wawakilishi wa wadi (MCA) zilizoko Kasarani, wakiongozwa na Pius Mwaura wa Zimmerman na Peter Warutere (Roysambu), walipuliza kipenga cha mipango ya ubomoaji huo kwa gavana Mike Sonko. Wengine walioshirikiana nao ni MCA wa Githurai Naftaly Mathenge na Antony Ng’ang’a, Kahawa West.

Gavana Sonko hakuchelea, na alifika na ujumbe wa afueni kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta, kukomesha ubomoaji huo. Alifichua kwamba kiongozi wa taifa ametangaza kusimamishwa kwa ubomozi wa majengo, hasa ya makazi Nairobi.

Soko hili lililobomolewa, sasa ni mahame. Picha/ Sammy Waweru

“Hakuna ubomoaji wa nyumba utakaofanywa tena Zimmerman. Ujumbe huu (akimaanisha ubomoaji wa majengo) tayari umemfikia Rais na mazungumzo kupata suluhu yatafanyika. Kila kitu kinachohusisha mradi wa shamba hili lazima kipitie afisini mwangu,” alisema gavana.

Licha ya wamiliki kuelekea mahakamani na kupata agizo la korti ubomoaji usitishwe, uliendelea.

“Nashukuru Rais Kenyatta kwa kuingilia kati suala hili. Mambo mengi yaliyofanywa yalipangwa na ‘watu wake’. Stakabadhi niliyopewa hapa inasema ni familia yake, watu wakome kuingiza jina la Rais katika hili,” alisema Bw Sonko.

Hapa ndipo ilipokuwa ofisi ya Zimmerman Settlement Scheme. Picha/ Sammy Waweru

Ubomozi uliofanyika Aprili 16, inasemekana Zimmerman Settlement Scheme ilikadiria hasara ya mali yenye thamani zaidi ya Sh1 bilioni. “Waliosimamia ubomozi walisema agizo la korti kuusimamisha ni makaratasi tu,” alilalamika mwenyekiti wa mradi huo, Bw Francis Kirima.

“Miongoni mwa ajenda kuu nne za Rais Kenyatta ni ujenzi wa makazi ya bei nafuu. Wahuni wanaotufanyia uhayawani huu wamebuni ajenda ya nne na tano, kubomoa na kunyakua, nia yao ni kuharibia Rais utendakazi wao,” alisema mwenyekiti huyo.

Gavana Sonko akihutubia wamiliki wa ploti na nyumba walioghadhabishwa na ubomozi wa makazi yao. Alisimamisha shughuli hiyo. Picha/ Sammy Waweru

Michael Ngugi, naibu katibu wa mradi huo, aliteta kuwa wakati wa ubomoaji askari waliosimamia walishirikiana na wahalifu mali yaibwe. “Maafisa waliokuwepo walilinda wezi kutuibia mali. Mbali na kubomolewa nyumba, wapangaji wetu walikadiria hasara kubwa ya mali yao kuporwa,” alisema Bw Ngugi.

Bi Elizabeth Karungari, mmoja wa wamiliki, alilalamikia kupoteza mali ya mamilioni ya pesa. “Hazina yangu yote ya kustaafu nilikuwa nimeiwekeza hapo, nitaanzia wapi?” alishangaa mama huyo.

“Wengi wetu tulichukua mikopo ili kununua ploti na kujenga. Hii ni hasara ambayo hatujui iwapo tutainuka tena kama maskwota,” alisema mmiliki mwingine, John Maina.

Mwenyekiti wa mradi wa shamba hilo, Francis Kirima akiongea mbele ya gavana Sonko na kumuonesha stakabadhi za umiliki wa shamba. Picha/ Sammy Waweru

Uhasama baina ya gavana Mike Sonko na seneta Johnson Sakaja ulionekana kuibuka hadharani, gavana akieleza kushangazwa kwake kimya cha Bw Sakaja.

“Nilipokuwa seneta mliniona nikitetea haki za wanyonge, kiasi cha kupigia Rais simu ubomoaji usimamishwe Kayole. Hii kazi ya kuongea Kizungu mingi bungeni haitusaidii. Seneta na wabunge waliochaguliwa wako wapi? Kwa kuwa seneta ameshindwa na kazi yake, nitaifanya kama gavana,” alisema.

Shamba hilo ni la karibu ekari 250 na Bw Sonko aliwataka wamiliki kushirikiana kwa karibu na madiwani ili kurahisisha afisi yake kupokea habari zinazolihusu. MCA wa Zimmerman Pius Mwaura, aliahidi kuhakikisha utata uliopo umetatuliwa, kauli iliyopigwa jeki na madiwani wenza.

Bw Mafaka, mmoja wa viongozi wa Zimmerman Settlement Scheme akiongea. Picha/ Sammy Waweru

Mradi huo una historia ya mizozo tangia 2002, ambapo una wahusika kadhaa wanaovutania shamba hilo.

Halmashauri ya kitaifa ya mazingira (Nema) na ya ujenzi (NCA), ndizo ziliidhinisha ujenzi wa nyumba katika shamba hilo linalositiri maelfu ya watu. Pia, hupokea huduma za stima na maji chini ya kampuni ya kusambaza nguvu za umeme nchini, KP na Nairobi Water & Sewerage Company.