Makala

Maswali mengi kuhusu ‘ulezi’ uliotumbukiza Wapwani kwa uraibu wa muguka

May 29th, 2024 4 min read

NA KALUME KAZUNGU

UTEPETEVU wa baadhi ya wazazi katika kufuatilia mienendo ya watoto wao umetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazotumbukiza vijana wengi Pwani kwenye uraibu wa kutafuna muguka.

Vijana ambao wamekuzwa katika mazingira au malezi ya kutendekezwa pia wameishia kutumia muguka, miraa, mihadarati na malevya mengine, ikiwemo pombe.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Msemaji wa Muungano wa Taireni Akwehu, Bw Karisa Kaingu aliwakosoa wazazi wanaowapa watoto wao, hasa wale waliobaleghe, uhuru mwingi kupita kiasi.

Taireni Akwehu ni vuguvugu linalowaunganisha Wapwani, hasa wale wa jamii ya Wamijikenda, kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook.

Bw Kaingu alisema hatua ya wazazi kuwapa watoto wao uhuru mwingi imewaacha vijana hao wakipotoka, hivyo kujiingiza kwenye uraibu wenye madhara tele.

Kauli yake inajiri wakati viongozi wa kaunti za Mombasa na Kilifi walikuwa wamepiga marufuku usafirishaji na matumizi ya muguka katika maeneo yao.

Viongozi wa kisiasa na kidini pamoja na wanachama wa mavuguvugu ya haki za binadamu wanadai uraibu uliokithiri Pwani wa kutafuna au kula muguka na miraa, unywaji wa pombe na uvutaji wa bangi na kunusa au kujidunga kokeni na heroni, umesababisha wengi kukosa dira maishani.

Bw Kaingu anasema punde kijana anapoachiliwa huru huishia kutangamana na marafiki wabaya ambao humrai kujiingiza kwenye uraibu na kuuharibu kabisa mwelekeo wake wa maisha.

Wauzaji wa muguka baada ya kuchukua bidhaa hiyo kutoka kwa lori lililoruhusiwa kuingia sokoni Kongowea, Mombasa mnamo Mei 29, 2024. Ni baada ya Mahakama Kuu ya Embu kusitisha kwa muda amri kuu za magavana wa Mombasa na Kilifi. PICHA | KEVIN ODIT

Mbali na malezi duni, Bw Kaingu alitaja bei rahisi inayouziwa fungu la muguka kuwa miongoni mwa misukumo inayowafanya vijana kutekwa kiurahisi na uraibu.

“Kigezo kikuu kinachotumbukiza Wapwani kwa uraibu wa muguka ni ulezi usiofaa. Endapo mzazi atampa mtoto wake misingi dhabiti ya maisha, sidhani mtoto au kijana huyo atayumbishwa na presha za marafiki hadi kuishia kuwa mraibu wa muguka, pombe na mihadarati,” akasema Bw Kaingu.

Aliongeza, “Ni rahisi kwa kijana kuanguka kwenye mtego wa muguka, hasa ikiwa hana maadili au misingi yoyote aliyopewa na mzazi au mlezi wake. Muguka wenyewe ni rahisi. Kwa Sh10 au Sh20 pekee, uko na kibunda chako cha muguka. Ni rahisi kuupata. Na ndio sababu Wapwani twazidi kuwapoteza vijana wetu wanaogeuzwa goigoi na huu muguka.”

Afisa huyo aidha aliikosoa serikali ya kitaifa, ikiongozwa na Rais William Ruto, kwa kupuuzilia mbali marufuku ya muguka yaliyokuwa yametolewa na baadhi ya magavana wa Pwani.

Magavana ambao tayari walikuwa wamepiga marufuku kuingizwa na kuuzwa kwa muguka kwenye kaunti zao ni Abdullswamad Sheriff Nassir wa Mombasa, Gideon Mung’aro wa Kilifi na Andrew Mwadime wa Taita Taveta.

Katika kikao cha Jumatatu kilichowakutanisha Rais Ruto na viongozi wa Embu wakiongozwa na Gavana Cecily Mbarire kwenye ikulu ya Nairobi, serikali ilitangaza marufuku hayo ya muguka yaliyoamriwa na baadhi ya kaunti za Pwani kuwa yasiyostahili.

Ni kwenye kikao hicho ambapo Rais Ruto pia alitangaza mpango wa kutenga Sh500 milioni kwenye bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2024/2025 katika kuboresha uzalishaji na uboreshaji wa zao hilo la muguka na miraa.

Nayo Jumanne, Rais aliweka chapisho kwa akaunti zake za mitandao ya kijamii kwamba baada ya mazungumzo ya simu na magavana wa Mombasa, Kilifi na Taita Taveta, walikuwa wamekubali kufanya kikao na maafisa kutoka Wizara ya Kilimo kutafuta muafaka kuhusu muguka.

Naye Jaji wa Mahakama Kuu ya Embu Lucy Njuguna aliamuru kwamba marufuku ya muguka Kilifi na Mombasa yasitishwe hadi Juni 8, 2024, kesi iliyowasilishwa na chama cha Kutherema muguka Sacco na Bunge la Embu itakaposikilizwa.

Lori la muguka baada ya kuruhusiwa kuingia sokoni Kongowea, Mombasa mnamo Mei 29, 2024. Ni baada ya Mahakama Kuu ya Embu kusitisha kwa muda amri kuu za magavana wa Mombasa na Kilifi. PICHA | KEVIN ODIT

Licha ya hao, Bw Kaingu anashikilia kuwa kuruhusiwa kuendelea kuuzwa kwa muguka na miraa na serikali ni jambo lisilofaa kwani linaangamiza kabisa jamii au kizazi kijacho.

“Nilikuwa nimefurahi pakubwa kuona kaunti zetu za Pwani zikianza kupiga marufuku biashara ya muguka. Rais Ruto naye amenivunja moyo kuruhusu zao hilo kuendelea kuuzwa Pwani. Kama tumeamua kupiga marufuku malevya nchini tusimame kidete kupiga malevya hayo yote. Tusiangalie tu kwamba muguka au miraa inainua uchumi au kuletea serikali kodi. Lazima muguka uangamizwe ili usiue kizazi chetu cha siku za usoni,” akasema Bw Kaingu.

Kauli ya Bw Kaingu iliungwa mkono na viongozi wa dini, wakiwemo mapadri, maimamu na maustadh kutoka Lamu na Pwani kwa ujumla, walioshikilia kuwa kinga ni bora kuliko kutibu.

Imamu wa Msikiti wa Jamia mjini Mokowe, Kaunti ya Lamu, Bw Mohamed Bwanamkuu alisema vijana wengi wanaugua akili punguani ilhali wengine wakiandamwa na msongo wa mawazo na jakamoyo ya kila mara kufuatia ulaji kwa wingi wa muguka na uvutaji bangi.

Watafunaji muguka ‘wakichonga’ baada ya kununua bidhaa hiyo sokoni Kongowea, Mombasa mnamo Mei 29, 2024. Ni baada ya Mahakama Kuu ya Embu kusitisha kwa muda amri kuu za magavana wa Mombasa na Kilifi. PICHA | KEVIN ODIT

Bw Bwanamkuu alisema hali hiyo itadhibitiwa vilivyo endapo marufuku ya muguka itaamriwa Pwani na Kenya kwa jumla.

“Vijana wamekuwa hawaambiliki wala kusemezeka mitaani. Hawawasikizi hata wazazi wao wenyewe. Yaani wamegeuka kuwa wenye akili punguani kutokana na ulaji muguka. Twapongeza marufuku iliyokuwa imetolewa dhidi ya muguka. Serikali ifikirie kuhusiana na janga hili la kupoteza vijana kwenye uraibu wa muguka,” akasema Bw Bwanamkuu.

Bi Fatma Ali, mzazi na mkazi wa kisiwa cha Lamu, alieleza wasiwasi wake kwamba endapo utumiaji muguka hautadhibitiwa huenda ukaathiri hata masomo shuleni.

Kulingana na Bi Ali, baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakijaibiwa kuingizwa kwenye uraibu wa muguka.

“Mara nyingi watoto wetu hatunao majumbani. Wako shuleni au mitaani, ambapo hutangamana na hawa watu wabaya wanaowapotosha kuingia kwenye uraibu wa muguka. Hili tayari tumelishuhudia mitaani kwetu kwani idadi ya watoto wanaoacha au kudinda kwenda shule inaendelea kuongezeka. Tuungane kupiga vita muguka,” akasema Bi Ali.

Mbali na kuwaacha vijana wakiathirika ubongoni, miraa pia husababisha walaji wake kuwa na mori, kusababisha msongo wa mawazo, mafadhaiko na mahangaiko ya kiakili.

Soma Pia: Viongozi wa kidini wataka muguka kupigwa marufuku kote nchini

Madhara mengine ya ulaji wa muguka na miraa ni kwamba hupunguza nguvu za kiume.

Utafiti uliofanywa Novemba 2015 kwa niaba ya serikali ya Kenya na wahadhiri wa chuo kikuu cha Moi kilichoko Bonde la Ufa, ulibaini kuwa majani ya miraa inayofahamika pia kama ‘Mairungi’ huzuia ukuaji wa mbegu za uzazi kwa wanaume.

Aidha ulaji wa kipindi kirefu wa miraa unafanya mbegu za kiume za wanaume kufa haraka pindi zinapoingia kwa mke wakati wanandoa wana malengo ya kupata mtoto.

Ulaji wa miraa pia huwa unasababisha mshtuko wa moyo au shinikizo la damu kwani mlaji baada ya muda wa matumizi huanza kuhisi damu yake ikienda kwa kasi.