Makala

Maswali Mkenya akifariki Saudia hotelini, ajenti akiingia mitini

Na KALUME KAZUNGU August 6th, 2024 2 min read

FAMILIA moja Kaunti ya Lamu imeachwa na maswali mengi kuhusu kifo cha ghafla cha jamaa yao aliyekuwa akifanya kazi nchini Saudi Arabia.
Bi Virginia Auma Hayoko, 32, anatoka kijiji cha Majengo Mapya, tarafa ya Witu, Kaunti ya Lamu.

Amekuwa akihudumu kama mfanyikazi wa nyumbani jiji kuu la Riyadh katika nchi hiyo ya Mashariki ya Kati tangu Septemba, 2022.

Mwili wa Bi Virginia hata hivyo ulipatikana kwenye chumba cha hoteli moja mjini humo Julai 6, 2024.

Katika mahojiano na Taifa Dijitali, ndugu, jamaa na marafiki walieleza kutamaushwa kwao na kifo hicho cha ghafla cha mpendwa wao katika nchi ya kigeni.

Bw Dickson Hayoko Mugari, ambaye ni nduguye mkubwa wa marehemu, aliiomba serikali kuingilia kati na kuchunguza kiini halisi cha kifo cha dadake.

Bi Virginia ni mama wa watoto wawili na alilazimika kusafiri Saudi Arabia miaka mitatu iliyopita katika harakati za kuwatafutia maisha wanawe, mamake, nduguze na dada zake.

Mmoja wa watoto wake yuko kidato cha kwanza katika shule ya sekondari ya Witu mjini, wa pili akiwa Gredi 6.

Bw Mugari Mugari alisema hali ya kifedha ni duni kwa familia yao kwa sasa, hivyo akaiomba serikali na wadau kujitokeza ili kuwasaidia kugharimia nauli ya kuusafirisha mwili kutoka Saudi Arabia hadi Kenya kwa mazishi.

“Tumeachwa bumbuazi tangu tulipofahamishwa kuhusu kifo cha Virginia. Alifariki Julai 6, 2024 akiwa hotelini nchini Saudi Arabia. Aliyetupigia simu kutujulisha ni mtoto wa dadangu ambaye pia anafanya kazi nchini humo. Alizungumza nasi Julai 13. Kifo cha dadangu ni pigo kubwa kwa familia yetu,” akasema Bw Mugari.

Mamake marehemu, Bi Susan Nabwire Akello, alisema kifo cha kitinda mimba wake kimesababisha dhiki kwa hali yake ya afya na pia hali ya familia kwa jumla.

“Alikuwa tegemeo kubwa kwangu. Watoto wake wako shuleni wakisoma kupitia fedha zake. Isitoshe, mimi, dada na ndugu zake hatuna kazi na tulimtegemea. Hatujui tutaanzia wapi. Tunaomba usaidizi kuurejesha mwili nyumbni kwa minajili ya mazishi,” akasema Bi Nabwire

Bi Christine Mugazi, dadake marehemu, alimlaumu ajenti aliyempeleka Bi Virginia Saudi Arabia kwa kujaribu kuwa msiri kuhusiana na kifo cha dadake.

Alilalamika kuwa tangu ajenti huyo alipokubali kwamba ni kweli Virginia alikuwa amefariki alijitenga kabisa na familia yake hasa kuhusiana na matayarisho ya kuurejesha mwili wa dadake Kenya kwa mazishi.

“Dadangu alipelekwa Saudi Arabia kupitia ajenti kwa jina Purity wa Shirika la usafiri la Pure Travel Recruitment Agency. Baada ya kifo cha dadangu kutokea, ajenti amekuwa akidinda kukubali. Baadaye ndipo akatuthibitishia kwamba ni kweli Virginia alikuwa amefariki. Tangu hapo ajenti huyo ameingia mitini na hataki mambo yoyote kutuhusu,” akasema Bi Mugazi.

Virginia Auma Hayoko, 32, ambaye ni mama wa watoto wawili, aliyefariki akifanya kazi nchini Saudi Arabia Julai 6, 2024. PICHA|HISANI