Maswali Ruto akifokea Museveni

Maswali Ruto akifokea Museveni

Na WANDERI KAMAU

URAFIKI baina ya Naibu wa Rais William Ruto na Rais Yoweri Museveni unaonekana kuingia doa baada ya kumfokea hadharani kiongozi huyo wa Uganda, Jumamosi.

Dkt Ruto alizungumza hayo katika msururu wa mikutano ya kisiasa nchini, akimtaka aachilie matrela kutoka Kenya yanayozuiliwa nchini Uganda bila masharti yoyote.

Matrela hayo yalinaswa wiki iliyopita yakiwa yamebeba samaki wa thamani ya Sh50 milioni katika wilaya ya Kasese, Uganda.

Dkt Ruto alisema ni vibaya kwa Uganda kuyazuilia matrela hayo, ilhali Kenya na Uganda ni majirani na wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

“Kuhusu samaki wanaoshikiliwa nchini Uganda, ningetaka kumwambia Rais Museveni kuwaachilia matrela hayo ili kuendeleza urafiki na ushirikiano wa EAC.

“Hiyo si bangi wala pombe haramu, bali ni bidhaa halali zilizokuwa zikisafirishwa na wafanyabiashara kutoka Kenya,” akasema Dkt Ruto. Naibu wa Rais alisema kukamatwa kwa matrela hayo kunatia taabani urafiki baina ya Uganda na Kenya.

“Hatuwezi kudai kuwa marafiki wazuri wakati sisi (Kenya) tunawaruhusu wafanyabiashara kutoka Uganda kufanya biashara nchini bila vikwazo vyovyote, lakini wenzetu wanakamatwa na kutozwa faini za juu au bidhaa zao kunaswa,” akasema Dkt Ruto.

Dkt Ruto alimshambulia Rais Museveni wiki tatu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukutana na mwanawe Rais Museveni, Jenerali Muhoozi Kainerugaba jijini Nairobi. Jen Muhoozi alimtaja Rais Kenyatta kama nguzo muhimu ya umoja wa Afrika Mashariki na barani Afrika.

“Ilikuwa heshima kubwa kumtembelea ndugu na shujaa yangu hivi majuzi jijini Nairobi. Rais Uhuru ni kielelezo bora kwa wengi Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla,” Jenerali Kainerugaba aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Jenerali Kainerugaba alikutana na Rais Kenyatta jijini Nairobi baada ya kuondoka nchini Somalia ambapo alizuru majeshi ya Uganda ya kudumisha amani chini ya Umoja wa Afrika (AU) kati ya Septemba 23 na 27, mwaka huu.

Jenerali Kainerugaba alikutana na Rais Kenyatta mwezi mmoja baada ya serikali ya Kenya kuzuia Dkt Ruto kusafiri nchini Uganda kwa sababu ‘hakuwa amepewa idhini na Rais Kenyatta’.

Ukaribu wa Dkt Ruto na Rais Museveni ulisababisha uhusiano baina ya Kenya na Uganda kudorora kiasi kwamba taifa hilo jirani limekuwa likipata kiasi fulani cha shehena ya mafuta nchini Tanzania.

Wadadisi wanahoji kwa nini Dkt Ruto hakutumia ukaribu wake na Rais Museveni kumshawishi kuachilia matrela hayo ya mafuta badala ya kumfokea katika mkutano wa siasa.

Mnamo 2015, Dkt Ruto alikuwa miongoni mwa viongozi waliomsaidia Rais Museveni kufanya kampeni za urais, ambapo aliibuka mshindi dhidi ya mpinzani wake wa muda mrefu, Dkt Kizza Besigye.

Julai mwaka huu, Dkt Ruto ndiye aliyekuwa mgeni wa heshima kwenye hafla ya kufungua kituo cha kutengeneza chanjo katika eneo la Matuga, wilaya ya Wakiso.Kwenye hafla hiyo, Dkt Ruto alisema nchi za Afrika zinapaswa kushirikiana katika kutatua changamoto zake kwa pamoja.

Upeo wa urafiki kati ya viongozi hao ulidhihirika 2019, wakati Chuo Kikuu cha Makerere kilipobuni Kitivo cha Mafunzo ya Masuala ya Afrika na Uongozi cha William Ruto. Hata hivyo, wadadisi wa siasa na mahusiano ya kimataifa wanasema kuna uwezekano uhusiano kati ya viongozi hao wawili umeanza kudorora, kwani si kawaida kwa Dkt Ruto kusikika akimfokea Rais Museveni.

“Ni hali inayoonyesha mwelekeo mpya wa mahusiano kati ya viongozi hao wawili. Ni hali itakayoendelea kujitokeza wazi hasa wakati uchaguzi mkuu wa 2022 unapoendelea kukaribia,” asema Dkt Godfrey Sang’, ambaye ni mtaalamu wa mahusiano ya kimataifa.

Kulingana na wadadisi, kuna uwezekano Rais Museveni ameanza kubadilisha msimamo wake, baada ya kikao kilichofanyika kati ya mwanawe na Rais Kenyatta mnamo Septemba. “Si nadra kwa msimamo wa Bw Museveni kuchangiwa na kikao hicho,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Kando na kuendeleza mikakati ya kisiasa anapolenga kuwania urais 2022, Dkt Ruto anadaiwa kumiliki msururu wa biashara kadhaa nchini Uganda.

Anadaiwa kumiliki mamia ya mashamba anakolima parachichi ambayo huwa anayauza barani Ulaya.

Anadaiwa pia kumiliki msururu wa vituo vya kuuzia mafuta.

Dkt Ruto vile vile anadaiwa kumiliki shamba la mpunga katika eneo la Bugiri, mashariki mwa taifa hilo.

“Katika hali ambapo Dkt Ruto anamiliki biashara kadhaa nchini Uganda na kumtegemea Rais Museveni kumsaidia kuendesha mikakati ya kisiasa kuvumisha azma yake kuwania urais, atapoteza pakubwa ikiwa patazuka mtafaruku kati yake na kiongozi huyo,” akasema Bw Mutai kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo.’

Dkt Matiang’i aliyekuwa akizungumza mjini Ol Kalou, Kaunti ya Nyandarua, alisema kuwa atatumia mamlaka yake kuhakikisha kwamba vituo vinavyotumiwa na wanasiasa kueneza chuki vinafungwa ili kuzuia fujo kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu ujao.

Alijitetea kwamba vituo vinavyoeneza chuki vitafungwa ili kudumisha amani nchini na wala si ishara ya kugandamiza uhuru wa vyombo vya habari.

“Ni jukumu la vyombo vya habari kuwa katika mstari wa mbele kuhubiri amani bila kuegemea mrengo wowote,” akasema Waziri Matiang’i.

Waziri huyo wa Usalama, alitoa onyo hilo huku visa vya wanasiasa kutumia wahuni kukabiliana na wapinzani wao vikionekana kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Naibu wa Rais William Ruto alikuwa kiongozi wa hivi karibuni msafara wake kushambuliwa na wahuni alipokuwa akijipigia debe mjini Busia.

Vijana hao waliofunga barabara kumzuia Dkt Ruto kuingia mjini Busia, walitawanywa na maafisa wa polisi wa kukabiliana na ghasia.

Jana, Dkt Matiang’i alisema kuwa tayari washukiwa wanane wamekamatwa kuhusiana na vurugu hizo.

Alisema washukiwa wengine waliohusika na ghasia hizo wangali wanasakwa na polisi.

“Sisi Wakenya tuliamua kukumbatia demokrasia. Hiyo inamaanisha kwamba tunasikilizana na kufanya kazi pamoja. Kutofautiana kimawazo miongoni mwa viongozi si sababu ya kutosha kusababisha vurugu na utovu wa amani nchini,” akasema Dkt Matiang’i.

You can share this post!

Serikali yashirikiana na FAO kuibuka na mpango maalum...

Hofu idadi ya walimu wanaokufa karibu na maeneo ya...

T L