Maswali Ruto akiidhinisha wawaniaji ugavana Pwani

Maswali Ruto akiidhinisha wawaniaji ugavana Pwani

Na WAANDISHI WETU

CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Naibu Rais William Ruto, kina kibarua kizito kuamua watakaowania uongozi wa kaunti za Pwani katika uchaguzi ujao.

Licha ya chama hicho kuhakikishia wanasiasa mara kwa mara kwamba kutakuwa na haki kuchagua wagombeaji wa UDA, Dkt Ruto aliidhinisha wazi baadhi ya wanasiasa wanaotaka kuwania ugavana wakati wa ziara yake Pwani.

Chama hicho kimefanya mkutano na wagombeaji watarajiwa leo Jumatatu jijini Mombasa, na inatarajiwa kwamba maafisa wa chama wamejitahidi kutuliza wasiwasi kuhusu uwezekano wa mapendeleo katika mchujo.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Dkt Ruto alimwidhinisha Naibu Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani, kurithi kiti cha Gavana Salim Mvurya. Wawili hao walichaguliwa kupitia kwa Jubilee.

Ijapokuwa Bi Achani alihudhuria mkutano ulioongozwa na Dkt Ruto, hakutangaza kujiunga na UDA.

Tikiti hiyo inawaniwa pia na Bw Mangale Lung’anzi.

“Namshukuru Mama Achani kwa sababu yeye atashikilia ile kazi ambayo ndugu yangu Mvurya amefanya. Sisi wote tunasema kazi iendelee,” akasema naibu rais.

Bw Mvurya ni mmoja wa magavana watatu wanaotumikia kipindi cha pili katika ukanda huo, wengine wakiwa ni Hassan Joho (Mombasa) na Amason Kingi (Kilifi).

Katika Kaunti ya Mombasa, Dkt Ruto alimwidhinisha aliyekuwa seneta Hassan Omar kuwania ugavana kupitia kwa UDA alipohutubu katika uwanja wa Allidina.

Baadhi ya wafuasi wa chama hicho humtaka Mbunge wa Nyali, Bw Mohamed Ali, ndiye apeperushe bendera ya UDA katika kinyang’anyiro hicho.

“Sisi kama mahasla Kenya nzima, tumejipanga kupambana na mabepari na mabwanyenye. Ni sisi mahasla ambao tutahakikisha tumeleta mabadiliko ya kiuchumi kwa manufaa ya kila Mkenya,” Bw Omar alisema Jumapili.

Mbunge wa Malindi, Bi Aisha Jumwa, kufikia sasa ndiye anayetarajiwa kuwa mgombeaji ugavana Kilifi kupitia UDA.

Hata hivyo, bado anakumbwa na kesi zinazohusu madai ya kushiriki ufisadi na mauaji, hali inayotishia azimio lake iwapo masuala hayo yatatumiwa dhidi yake na wapinzani.

“Tuingie katika mambo muhimu ambayo yanatuumiza. Kwanza tuwekane wazi kuhusu njaa hapa Kilifi, hatujawahi kuona gavana Amason Kingi hata siku moja akija mahali hapa na kuwauliza wala kuwaletea chochote,” alisema Bi Jumwa, wakati wa mkutano wa UDA Kilifi.

Katika Kaunti ya Lamu, mwanzilishi wa shirika la kutoa misaada ya kimatibabu la Safari Doctors, Bi Umra Omar ndiye ameonyesha nia ya kuwania ugavana kupitia kwa UDA.

Dkt Ruto alipokuwa Kaunti ya Taita Taveta, imebainika alikutana na aliyekuwa Gavana John Mruttu na Bw Stephen Mwakesi ambao wote wanawania tikiti ya UDA wakitaka kumwondoa Gavana Granton Samboja mamlakani.

Duru zilisema mkutano huo ulinuiwa kuwapatanisha ili kuwe na mgombeaji mmoja, kuzuia mpasuko chamani.

Hata hivyo, mratibu wa UDA katika kaunti hiyo, Bw Scaver Masale, alisema hakuna aliyeshinikizwa kuweka kando maazimio yake ili kuunga mkono mwenzake.

Katika mahojiano ya awali, Mbunge Mwakilishi wa Wanawake kaunti hiyo, Bi Lydia Haika, alisema kuna mazungumzo yanaendelea ili Mabw Mruttu na Mwakesi wakubaliane kushirikiana.

“Wakishindwa kukubaliana basi watalazimika kuingia katika kura ya mchujo ambayo itakuwa huru na wa haki,” Bi Haika aliambia Taifa Leo.

Ripoti za Siago Cece, Alex Kalama, Lucy Mkanyika na Valentine Obara

You can share this post!

TANZIA: Colin Powell afariki

ODONGO: Tusifuate vyama 2022 ila falsafa za wawaniaji

F M