Habari Mseto

Maswali tata kuhusu Mswada wa Fedha 2024

Na Na DAVID MWERE June 17th, 2024 1 min read

BUNGE la Kitaifa wiki hii litaanza mjadala kuhusu Mswada wa Fedha wa 2024 huku maswali yakizuka kuhusu uhalali wa Kikatiba wa baadhi ya sheria ambazo mswada huo unalenga kubadilisha.

Hii ni baada ya kubainika kuwa baadhi ya sheria ambazo zinalengwa, zinaweza kubadilishwa tu kupitia mchango wa Bunge la Seneti.

Kamati ya Fedha na Mipango inatarajiwa kuwasilisha mswada huo bungeni baada ya kukamilisha kupokea maoni kutoka kwa umma, shughuli ambayo ilichukua wiki mbili.

Mashirika 500 na Wakenya waliwasilisha maoni yao kuhusu mswada huo.

Mswada wa Fedha 2024 unalenga kubadilisha sheria 10 na inakadiriwa kuwa utachangia kupatikana kwa Sh347 bilioni za ziada ambazo zitatumika kufadhili bajeti ya Sh3.9 trilioni. Bajeti hiyo iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha Profesa Njuguna Nd’ungu wiki jana.

Sheria ambazo zinalengwa kubadilishwa ni ile ya Ushuru wa Ziada, Ushuru kwenye Bidhaa, Ushuru wa Mapato, Sheria kuhusu Kanuni za Ukusanyaji wa Ushuru pamoja na Sheria ya Ada na Matozo.

Hata hivyo, kujumuishwa kwa Sheria ya Nyumba za Gharama Nafuu na ile ya kulinda data, kunatishia uhalali wa Kikatiba wa mswada huo iwapo utapitishwa na kuwa sheria.

Hii ni kwa sababu Mkenya yeyote anaweza kuelekea kortini kupinga sheria hiyo kutokana na kutohusishwa kwa seneti katika kupitishwa kwake.

Aidha, pendekezo la kujumuisha ushuru wa asilimia 2.5 kwenye kilomita ambazo gari limekimbia, kupitia kubadilishwa kwa sheria ya ushuru wa mapato, limeibua maswali.

Hii ni kwa sababu jukumu hilo ni la serikali ya kaunti.

“Kabla Bunge kutathmini mswada huo, Maspika wa Bunge la Kitaifa na Seneti wanastahili kuafikiana iwapo ni mswada unaohusu kaunti.”

Hapo jana, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula na mwenzake wa Seneti Amason Kingi hawakujibu maswali ya Taifa Leo kuhusu utata huo.

Haijabainika iwapo wawili hao wameshakutana na kuzungumzia mswada huo tata au la.