Makala

Maswali visa vya moto shuleni vikiongezeka Kilifi

February 4th, 2024 2 min read

NA ALEX KALAMA

BWENI moja la Shule ya Upili ya Mariakani katika Kaunti ndogo ya Kaloleni limeteketea kwa moto.

Bweni la Mississippi liliteketea Jumamosi usiku chanzo kilichosababisha moto huo kikiwa bado hakijabainika kufikia sasa.

Miale ya moto ilionekana juu ya anga kutoka kwenye shule hiyo katika mji wa Kaloleni.

Mkasa huo ulitokea siku mbili tu baada ya bweni moja kuchomeka hadi kuwa majivu katika Shule ya Upili ya Wasichana ya St John’s ambayo pia iko Kaloleni.

Matroni katika shule hiyo ya St John’s alikamatwa kuhusiana na kisa hicho cha moto.

Shule hiyo ilifungwa na wanafunzi wanatarajiwa kurejea shuleni upya Jumatatu.

Visa vya uchomaji shule vinaendelea kushuhudiwa kwenye Kaunti ya Kilifi.

Shule nyingi za upili katika kaunti hiyo ziliandikisha matokeo duni kwenye Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne mwaka 2023.

Mwaka 2023 shule mbili zilichomeka katika Kaunti ndogo ya Ganze na mwaka huu 2024 shule mbili zimechomwa katika Kaunti ndogo ya Kaloleni katika kaunti hiyo ya Kilifi.

Wenyeji na wakazi wanahisi ipo haja ya wadau wa elimu, maafisa wa usalama na wazazi kuweza kuinamisha vichwa vyao pamoja kuibuka na mbinu zitakazowezesha kujua sababu zinazochangia kufanyika kwa visa hivi na kisha kuangalia njia au namna ya kuzuia jambo hili kutokea tena.

Kilifi ni mojawapo ya zile kaunti ambazo idadi kubwa ya wazazi hawana uwezo wa kumudu kuwalipia karo watoto wao.

Ndiposa wengi wamekuwa wakitegemea misaada kutoka kwa wahisani mbalimbali kufadhili masomo ya watoto wao.

Pia Kaloleni na Ganze ambao visa hivi vya uchomaji shule vimeshuhudiwa, ni baadhi ya yale maeneo ambayo hukumbwa na ukame mara kwa mara katika kaunti hiyo.

Shule nyingi za Kaloleni na Ganze bado majengo na miundomsingi yake mingine ni duni inayohitajika kuboreshwa.

Uchomaji wa shule unazidi kurudisha nyuma juhudi za uboreshaji wa viwango vya elimu Kilifi.

Swala hili la uchomaji wa shule limezidi kuwa kitendawili kisichokuwa na jibu kwa wazazi wengi Kaunti ya Kilifi ambao bado wanajikuna vichwa wakifikiria na kuwaza wapi watatoa pesa za kupeleka watoto wao kujiunga na Kidato cha Kwanza.

Huku ugumu wa maisha na ukosefu wa fedha ukiwa unawakeketa maini, sasa mzigo mwingine unawaandama kutokana na shule kuchomwa.