Habari MsetoSiasa

Maswali yaibuka kuhusu upinzani kumezwa na serikali

December 13th, 2018 1 min read

Na WANDERI KAMAU

VIONGOZI wote wa Upinzani Jumatano waliungana na Rais Uhuru Kenyatta kuadhimisha Sikukuu ya Jamhuri katika Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo, Nairobi hali iliyozua maswali ikiwa hatimaye “wamemezwa” na serikali.

Hii ni kinyume na hafla za awali, ambapo baadhi yao wamekuwa wakisusia kuhudhuria.

Kando na kiongozi wa ODM Raila Odinga, ambaye amebuni mwafaka wa kisiasa na Rais Kenyatta, viongozi wengine wa muungano wa NASA pia walionekana kushabikia muungano huo mpya.

Wale waliohudhuria ni kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, Kalonzo Musyoka (Wiper) na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula, ambaye pia ndiye kiongozi wa chama cha Ford Kenya.

Baada ya kukagua gwaride la heshima alilokuwa ameandaliwa na wanajeshi, Rais aliwasalimia viongozi hao, walioketi kandokando kabla ya kuketi katika kiti chake rasmi.

Hasa, Bw Kenyatta alionekana kufurahishwa na Bw Odinga, ambaye alimpigia saluti licha ya kuvaa mavazi ya kijeshi.

Upekee mwingine wa hafla hiyo ni kwamba ilikuwa mara ya kwanza kwa Bw Wetang’ula kuhudhuria hafla ya kitaifa, kwani amekuwa miongoni mwa wakosoaji wakubwa wa uongozi wa Bw Kenyatta, akiutaja kuegemea ufisadi na kuendeleza ukabila.

Bw Wetang’ula, ambaye ametangaza nia ya kuwania urais, pia amekuwa akikosoa mwafaka kati ya mabw Kenyatta na Odinga, akiutaja kutowashirikisha Wakenya wote.

Pia amekuwa akimkosoa Bw Odinga kuwa “msaliti” kwa kubuni mwafaka huo “kisiri” bila kuwaarifu wanachama wengine wa muungano huo.

“Hatua ya Bw Odinga kuondoka katika NASA bila kuniarifu, wala wanachama wengine ni ishara ya wazi kwamba aliongozwa na maslahi yake binafsi, ila si lengo la kuwaunganisha Wakenya,” akasema.

Bw Mudavadi vile vile amekuwa mkosoaji wa serikali, akiapa kubaki upinzani, hata ikiwa atabaki peke yake.

“Sitawasaliti Wakenya. Nitaendelea kuikosoa serikali kama sauti yao m kwani inaonekana kuwa kila mmoja anapania kuingia serikalini,” akasema Mudavadi.

Bw Musyoka tayari ametangaza wazi kwamba atashirikiana na Bw Kenyatta kuwahudumia Wakenya.